NEWS

Tuesday 15 June 2021

DC Bupilipili: Njooni Bunda kuna fursa za kipekee





MKUU wa Wilaya (DC) ya Bunda mkoani Mara, Mwalimu Lydia Bupilipili amewahimiza wawekezaji nchini kuchangamkia fursa lukuki za uwekezaji zinazopatikana katika sekta ya utalii, wilayani humo.

 

DC Bupilipili ametoa wito huo leo Juni 15, 2021 wakati akizungumza katika kongamano la kutangaza fursa za uwekazaji wilayani humo, lililofanyika katika Chuo cha Uwalimu Bunda (BTC).
 

Ametaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni hoteli za kitalii, michezo ya ziwani, kupanda mlima Balili ambao unawezesha wageni kutazama Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na fukwe za Ziwa Victoria.

“Bonasi ya kuwaona wanyama kabla ya kulipia inapatikana Bunda pekee, njooni mjenge hoteli za kitalii, mtu anayetaka kutalii, aogelee hadi achoke, aje Bunda au atembelee Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa urahisi, au apande mlima atakaoona ziwa na wanyama kwa wakati mmoja, aje hapa [Bunda],” amesema DC Bupilipili.

"Maeneo ya kuwekeza yamejaa na usalama upo wa kutosha, yeyote atakayeonesha kuwa anataka kuwekeza Bunda katika sekta ya yoyote tutamlinda,” amesisitiza katika kongamano hilo.

Awali, akifungua kongamano hilo, Kaimu Mkuu wa Mkoa Mara, Dkt Vicent Naano amesema kwamba licha ya eneo kubwa la Hifadhi ya Serengeti lipo mkoani Mara, wakazi wake hawajachangamkia ili kunufaisha hiyo, kama ambavyo mikoa mingine ya Arusha na Kilimanjaro inanufaika.

Dkt Naano akifungua kongamano hilo

“Huu mkoa ulikuwa umefungwa, yaani watalii wakija hawashukii hapa, kuitafuta TANAPA hadi uwende Arusha, unakuta wilaya kama Tarime ipo mpakani watalii wanapita tu, sasa tumieni fursa zilizofunguliwa kuutajirisha mkoa huu,” amesema Dkt Naano.

Ameitaka wilaya hiyo kuhakikisha inaunda kamati itakayofuatilia masuala yote ya utalii na uwekezaji, ambayo itakuwa inakutana kila baada ya miezi miwili, chini ya Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) wa Mara.

Naye Afisa Mhifadhi Mkuu na Mkuu wa Kitendo cha Utalii wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Tutindiga George amewashauri wawekezaji kama wanataka biashara ya utalii ichangamke katika eneo hilo, wajenge hoteli nyingi na kambi za kitalii (camp sites).

“Bunda wajipange sawasawa upande wa malazi na hoteli, kwani yapo maeneo mengi ya kuwekeza camp sites ili wageni wasikose sehemu za kulala, pia wana Bunda tukubaliane tukae pamoja tuinue utalii katika ukanda huu,” amesema Mhifadhi Tutindiga.


Mhifadhi Tutindiga George



Baadhi ya washiriki wa kongamano hilo
 

Aidha, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Mara, Boniface Ndengo amewambia washiriki wa kongamano hilo kuwa Rais wa TCCIA Taifa amemtuma kuja hapo kutazama fursa zilizopo ili waanze kujenga viwanda na hoteli.

“Baada ya kongamano hili rais wa chemba ya wafanyabiashara taifa ameniambia kwamba atawaleta wawekezaji rasmi kuja kutembelea maeneo ya kuwekeza hoteli na viwanda,” amesema Ndengo.

 

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages