NEWS

Tuesday 15 June 2021

RAS Gabriel awahimiza madiwani Serengeti kufuatilia fedha na miradi ya serikali kwa maendeleo ya wananchi




MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, wametakiwa kuongeza juhudi katika kufuatilia na kusimamia fedha na miradi ya serikali, na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na maendeleo ya kisekta.

Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) wa Mara, Albert Gabriel ameyasema hayo katika kikao maalum cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo, kilichofanyika mjini Mugumu, leo Juni 15, 2021.

Kikao hicho kimeongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Nurdin Babu aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Salum Hapi, kwa ajili ya kupitia hoja na maoni ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa halmashauri hiyo.

Katika hotuba yake, RAS Gabriel amewataka madiwani na watendaji wa halmashauri hiyo kuimarisha umoja, upendo na ushirikiano katika kusimamia miradi ya maendeleo ya wananchi.


RAS Gabriel akihutubia kikao hicho

“Bila umoja hatuwezi kutoka… Mkipendana na kushirikiana, mtakosoana, mtaelekezana kistaarabu, mtakuwa wazazi na walezi wazuri wa halmashauri hii,” Gabriel amesisitiza.

Kwa upande mwingine, Gabriel amewataka watumishi wa idara za manunuzi na ukaguzi wa ndani katika halmashauri hiyo kuongeza umakini katika utendaji wao, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kila manunuzi yanafanyika kwa kufuata taratibu, kanuni na sheria zilizopo.

RAS huyo amesisitiza hayo kutokana na ripoti ya ukaguzi uliofanywa na CAG, kubaini kuwa baadhi ya matumizi ya fedha za serikali katika halmashauri hiyo hayana vielelezo.

Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayub Mwita Makuruma amesema hoja na maoni ya CAG vimewaongezea madiwani ari ya kushirikiana na watendaji katika kuimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha za umma.


Makuruma akiahidi ushirikiano wa madiwani na watendaji

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa, Babu, ameipongeza kamati ya fedha, uongozi na mipango, kama si madiwani wa halmashauri hiyo kwa ujumla, kwa kuunga mkono maoni ya CAG ambayo yameelekeza hatua za kufuata ili kuweka mambo sawa.


Babu akipongeza madiwani

Hata hivyo, awali, Mkurugenzi Mtendaji, Mhandisi Juma Hamsini, amekieleza kikao hicho kwamba halmashauri hiyo haijapata hati chafu kwa miaka tisa mfululizo.


Hamsini akizungumza kikaoni

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages