NEWS

Wednesday 2 June 2021

DC Msafiri ataka uchenjuaji madini utengewe maeneo maalumu kuepusha uchafuzi wa vyanzo vya maji




Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri (aliyesimama) akifungua mkutano wa Jukwaa la Wadau wa Dakio la Mara, mjini Tarime leo.

MKUU wa Wilaya (DC) ya Tarime mkoani Mara, Mhandisi Mtemi Msafiri amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zinazounda wilaya hiyo [Tarime Vijijini na Tarime Mji] kutenga maeneo maalumu ya shughuli za uchenjuaji wa madini kuepusha uchafuzi wa vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla.

Mhandisi Msafiri ametoa agizo hilo wakati akifungua mkutano wa Jukwaa la Wadau wa Dakio la Mara, mjini Tarime, leo Juni 2, 2021, na kuelekeza wakurugenzi hao kuwashirikisha maofisa mazingira wa halmashauri hizo katika utekelezaji wa agizo hilo.

 

Lengo la mkutano huo ni kuchochea ushiriki wa wadau katika usimamizi endelevu wa maji kwa ajili ya kizazi cha sasa na vijavyo.


Washiriki wa mkutano huo wakifuatilia mada katika ukumbi wa Blue Sky mjini Tarime

DC Msafiri ametumia nafasi hiyo pia kupiga marufuku shughuli za uchenjuaji wa madini kwenye makazi ya watu wilayani Tarime, kwa sababu zinachangia uchafuzi wa mazingira na vyanzo vya maji.

“Utunzaji wa vyanzo vya maji ni muhimu kwa sababu maji hayana mbadala katika maisha ya binadamu na viumbe hai wengine,” DC Msafiri amesema.


DC Msafiri (wa tatu kutoka kushoto waliokaa) katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali na washiriki wa mkutano huo.

Mhandisi Msafiri amesisitiza kuwa kila mtu ana wajibu wa kutunza vyanzo vya maji na kuepuka vitendo vya uharibifu wa mazingira ukiwemo ukataji miti ovyo.

Aidha, ameshauri washirikiki wa mkutano huo kuweka maazimio machache yanayotekelezeka kwa ajili ya usalama wa vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla.

Awali, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB), Dkt Renatus Shinhu ametaja vyanzo muhimu vya maji katika bonde hilo kuwa ni pamoja na Ziwa Victoria, Mto Mara na Mto Mori.

“Mto Mara ni tegemeo muhimu la ikolojia ya Serengeti,” ameongeza.


Dkt Shinhu (aliyesimama) akizungumza katika mkutano huo

Dkt Shinhu ametaja mada zinazowashilishwa kwenye mkutano huo ulioandaliwa na LVBWB kuwa ni Ijue Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria na Dakio la Mara, Mpango wa Kugawana Maji (WAP) na Kanuni zake, vibali vya matumizi ya maji na tozo mbalimbali.

Mada nyingine ni shughuli mbalimbali za uhifadhi na utunzaji wa rasilimali za maji zinazofanywa na wadau katika Dakio la Mara Mori.

Washiriki wa mkutano huo ni viongozi wa idara za maji, mazingira, misitu, jumuiya za watumia maji, wachimbaji madini, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, miongoni mwa wadau wengine wa maji, wakiwemo kutoka maeneo ya ikolojia ya Serengeti.

(Habari na picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages