NEWS

Monday 28 June 2021

Gari jipya la wagonjwa Tarime Vijijini lapata ajali, mmoja afa
GARI jipya la kubeba wagonjwa (ambulance) la Hospitali ya Nyamwaga katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) mkoani Mara, limepata ajali na mtu amesemekana kupoteza maisha katika ajali hiyo.

Gari hilo aina ya Land Cruiser lenye namba DFPA 8550, lilitolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto - kupitia kwa Mbunge wa Tarime Vijiji, Mwita Waitara ambaye alilikabidhi katika halmashauri hiyo, Juni 4, mwaka huu.

Taarifa zilizoifikia Mara Online News kutoka ndani ya halmashauri hiyo leo, zimesema gari hilo lilipata ajali saa tisa usiku wa kuamkia jana Juni 27, 2021 katika barabara ya Igoma jijini Mwanza, wakati likisafirisha mgonjwa na watu wengine wawili kutoka zahanati ya Nyangoto iliyopo Tarime Vijijini kwenda Hospitali ya Rufaa Bugando.


Mbunge Waitara akifurahia kupokea gari hilo, siku chache kabla ya kulikabidhi


Linavyoonekana baada ya ajali

Kwa mujibu wa taarifa hizo, aliyefariki dunia katika eneo la ajali hiyo ni ndugu wa mgonjwa huyo, aliyekuwa akimsindikiza kwenda Bugando.

“Dereva wa gari hilo na watu wengine wawili waliokuwa ndani ya gari hilo wametoka salama,” kimesema chanzo chetu cha habari.

Hata hivyo, Mara Online News inaendelea na juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, kwa ajili ya kuweka wazi jina la marehemu na chanzo cha ajali hiyo.

(Imeandikwa na Mara Online News)

1 comment:

  1. Poleni kwa hilo lililotupata pia twajivunia kuwa na wanahabari Mara

    ReplyDelete

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages