NEWS

Monday 7 June 2021

Mkaa, migodi ya madini vinavyoangamiza mazingira bonde la mto Mara



MKAA ni kitega uchumi kwa wananchi wa mkoa wa Mara. Lakini uzalishaji wake unatajwa kuchangia uharibifu wa mazingira ambayo ni muhimu kwa maisha ya binadamu na viumbe hai wengine.

John Mniko (sio jina lake halisi), anaishi kwa kutegemea biashara ya mkaa.

“Hii kazi ya kusaka mkaa ni ngumu, lakini inabidi niifanye ili kupata kipato kwa ajili ya mkate wa familia,” Mniko ameambia Mara Online News, huku akiwa amebeba magunia kadhaa ya mkaa kwenye pikipiki wilayani Butiama, hivi karibuni.

Ameongeza “Huwa tukifika vijijini tunakusanya mkaa kwa watu wanaochoma (wazalishaji) na kwenda kuuza mjini Musoma.”

Kwa mujibu wa Mniko, gunia la mkaa linauuza hadi Sh 70,000 katika soko la Musoma.
Wananchi wakisafirisha mkaa kutoka vijijini kwenda mjini Musama

Hivyo, Musoma ni moja ya miji ya mkoa wa Mara inayotegemea mkaa ambao chanzo chake ni miti iliyopo katika maeneo ya bonde la mto Mara.

Uzalishaji wa mkaa unaripotiwa kuangamiza miti mingi ya asili katika bonde hilo, hali inayohatarisha uhai wa ikolojia ya Mara.

“Miti ya asili ilikuwa mingi katika maeneo yetu, mfano katika kijiji cha Kwisaro, lakini hivi sasa imepungua sana,” anasema Mwenyekiti wa jumuiya ya watumia maji Mara Kusini.

Jumuiya hiyo inaundwa na vijiji kadhaa vinavyopakana na bonde la mto Mara katika wilaya ya Butiama.

Baadhi ya vijiji hivyo ni Wegero, Kwisaro na Kirumi. Mairi anasema baadhi ya vijiji kikiwemo Wegero, bado kuna misitu ya asili ambayo hivi sasa inashambuliwa kutokanaa na sababu za kiuchumi.

“Sio tu mkaa miti mingi pia inakatwa na kwende kwenye migodi kwa ajili ya shughuli za uchimbaji na hili nalo ni tatizo,” anasema Mairi.

Mairi anaongeza “Mahitaji makubwa ya miti ni kwa ajili ya kuni, mkaa na kwenye migodi.”

Wananchi wanaoishi jirani na bonde la mto Mara wanaiomba serikali kuwa na mpango wa kupunguza matumizi ya mkaa na kuni ili kunusuri mazingira.

“Suluhisho ni nishati mbadala kama vile matumi ya gesi. Kinachotakiwa ni kupunguza bei ya gesi ili wananchi wengi waweze kumudi kutumia gesi,” anasema Tatu Stephen ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kwisaro.

Anaongeza “Kama gesi haitapungua bei, miti itaisha na mazingira yataharibika.”

Tatu analalamika kuwa hata matumizi ya kuni yamekuwa yakiwasababishia madhara makubwa ya kiafya, hasa kufifisha uoni wa macho.

“Wanawake wengi nikiwemo mimi sioni vizuri, na pengine ni kwa sababu ya moshi wa kuni,” anasema Tatu.

Hata wauuza mkaa wanakiri kuwa hivi hasa wanapata mkaa kwa shida baada ya miti kupungua.

“Misitu imepungua sana na mkaa pia unapungua,” anasema Mniko, huku akihangaika kusafirisha magunia kadhaa ya mkaa kwenye pikipiki kutoka kijiji cha Wegero kwenda mjini Musoma.

Biashara ya mkaa inategemewa na vijana wengi katika vijiji vya wilaya mbalimbali za mkoa wa Mara kama ilivyo kwa Mniko.

Hata hivyo, serikali za wilaya zimekuwa zikipiga marufuku uchomaji na biashara ya mkaa kwa lengo la kunusuru mazingira.

Simon Odunga, Mkuu wa Wilaya ya Rorya, ni miongoni mwa viongozi wa serikali ambao wametangaza operesheni kali dhidi ya biashara ya mkaa katika eneo lake la uwatala.

“Uchomaji mkaa unaharibu sana mazingira Rorya, tuache mkaa,” Odunga amekuwa akikaririwa na vyombo vya habari akisisitiza kuwa uchamoaji wa mkaa sio shughuli halili.

Baadala yake, Odunga amekuwa akitawataka wananchi wa wilaya hiyo ambayo pia baadhi ya vijiji vyake vipo ndani ya bonde la mto Mara, kuanzisha shughuli halalili za kiuchumi ikiwemo kilimo cha mazao ya biashara na chakula, au kilimo cha bustani.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa wananchi wengi waliopo jirani na eneo oevu la Mto Mara na maeneo mengine wanalazimika kuchoma mkaa kutokana na kukosa njia nyingine ya kupata kipato cha kujikumu na familia zao.

Mfano, ukosefu wa zao la biashara la uhakikka katika wilaya ya Rorya, unaelezwa kuchangia uchomaji wa mkaa katika wilaya hiyo, ambayo huenda inaongoza kwa kuzalisha mkaa mkoani Mara.

“Wananchi wengi wanachoma mkaa kama sehemu ya kujipiatia kipato kcha ujikimu kimaisha, hawana njia nyingine za kupata kipato. Uchomaji ni mkubwa, karibu wilaya yote hata katika eneo la Mara Sibora, ambalo ni jirani na mto Mara,” anasema Siproza Charles ambaye ni Mwenyeketi wa jumuiya za watumia maji Mara Kusini.

Siproza anasema wananchi wa wilaya hyo wanalima mazao kwa ajili ya chakula tu bila ziada ya kuuza kwa ajili ya matumizi mengine, jambo linalowafanya waendelee kutegemea mkaa kwa ajili ya kujipatia kipato.

“Ili wapate pesa ya mboga na mahitaji mengine yakiwemo ya watoto kwenda shule, wananchi wanategemea mkaa,” anaongeza.

Siproza ambaye ni miongini mwa wananchi wanaojitolea kulinda na kuhamasisha uhifadhi endelevu wa bonde la mto Mara, anashauri uanzishaji wa mazao ya biashara katika wilaya hiyo, kama njia mbadala ya kujipatia kipato.

“Wananchi wapatiwe njia mbadala ya kujipatia kipato, badala ya kutegemea mkaa, inaweza kuwa mazao ya bishara na kilimo cha mboga mboga,” mama huyo ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mara Sibora, ameiambia Mara Online News.

Katika hatua nyingine, Sauti ya Mara imedokezwa kuwa serikali ina mpango wa kuanzisha teknolojia itakayopunguza matumizi ya miti katika mashimo ya wachimbaji wa migodi midogo mkoani Mara.

Wataalamu wa mazingira kutoka serikalini wanasema elimu inatakiwa kuendelea kutolewa kwa wananchi na kuimarisha utendaji kazi wa kamati za mazingira ngazi ya vijiji.


Magogo ya miti iliyokatwa kandokando ya mto Mara mkoani Mara

“Ukataji miti katika maeneo ya bonde la mto Mara bado ni tatizo na miti ya asili imeisha katika baadhi ya vijiji. Kinachotakiwa ni kamati za mazingira na serikali za vijiji kusimamia uhifadhi wa mazingira katika maeneo yao,” Ofisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Martha Mahule anasema.

Martha anaongeza “Sheria inazipa serikali za vijiji mamlaka ya kusimamia uhifadhi wa mazingra katika maeneo yao.”

Ofisi ya Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) ya Mjini Musoma imekuwa ikitoa elimu juu ya mazingira katika vijiji vilivyo jirani na mto Mara na kupanda miti ili kutunza mazingira.

“Mbali na kupanda miti, tunatoa elimu kwa wananchi wasikate miti ovyo na wakikata mita wapende miti, yaani kata mti panda mti,” Afisa wa Maji Dakio la Mara-Mori, Mhandisi Mwita Mataro anasema katika mazungumzo na Sauti ya Mara.

Mhandisi Matato anasema, hivi karibuni ofisi yake imepanda maelfu ya miti katika maeneo yaliyo jirani na mto Mara.

“Mfano, mwezi wa tatu pekee mwakaa huu tumepanda miti 5,000 katika maeneo mbalimbali na tunashirikisha jamii,” anasema Mhandisi Mataro.

Kaulimbiu ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu inasema “Tutumie Nishati Mbadala: Kuokoa Mfumo wa Ikoloji”.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages