NEWS

Friday 18 June 2021

Wadau mkoani Mara waandaa bonanza kuhamasisha utalii wa ndani Serengeti
WADAU wa sekta ya utalii mkoani Mara wameandaa bonanza maalum la kuhamasisha utalii wa ndani litakalofanyika Juni 26, 2021 kwenye uwanja wa Karume mjini Musoma, wakilenga kuandikisha wananchi wanaohitaji kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Akizungumza na Mara Online News mkoani hapa hivi karibuni, Mratibu wa bonanza hilo, Albert Chenza amewataja wadau hao kuwa ni NCT Twende Kutalii, Serengeti Safari Marathon na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ambao wameshirikiana kuandaa safari ya kutalii katika hifadhi hiyo, Julai 3, 2021.

“Bonanza hilo litaanza asubuhi hadi saa 12 jioni na tutalitumia kuuza tiketi kwa bei punguzo ya kwenda kutalii mbugani kwa gharama ya shilingi 49,000, ambayo itajumuisha usafiri wa kwenda na kurudi, chakula na kiingilio cha hifadhi hadi jioni,” amesema Chenza.

Ameongeza kuwa katika bonanza hilo, kutakuwa na michezo mbalimbali, ikiwemo ya riadha, kuvuta kamba, wasanii kuonesha sanaa zao, ambapo kwa upande wa soka, mshindi wa kwanza atapewa zawadi ya medali, jezi za Serengeti na shilingi laki mbili.

“Timu zitakazoshiriki soka ni ya Bodaboda, Bajaji, Musoma Veterani na Biashara Veterani, wakati mshindi wa pili atajinyakulia shilingi laki moja na nusu, na mshindi wa tatu atapewa jezi za Serengeti,” amesema Chenza.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages