NEWS

Thursday 17 June 2021

Kemanyanki Group wafanikisha uratibu wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika Nyamongo


KIKUNDI cha Kemanyaki, jana kimefanikisha uratibu wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika katika vijiji vinavyozunguka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, uliopo Nyamongo wilayani Tarime, Mara.

Maadhimisho hayo yamefanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya Ingwe, nje kidogo ya mji mdogo wa Nyamongo na kuhudhuriwa na mamia ya watoto na wadau wanaoshugulika na masuala yanayohusu ustawi wa watoto.

“Kama kikundi cha kijamii, tumefurahi kushirki katika kuratibu maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika hapa Nyamongo kwa mwaka huu, na tutaendelea kushirikiana na wadau wengine kutatua changamoto zinazowakabili watoto ili wafikie ndoto zao kielimu,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Kemanyanki Group, Nicolaus Mgaya, muda mufupi baada ya madhimisho hayo ambayo yamefadhiliwa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, ambao kwa sasa unaendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania - kupitia kampuni ya Twiga Minerals.Mkurugenzi Mtendaji wa Kemanyanki Group, Nicolaus Mgaya.

Madhimisho hayo yamefanyika wakati kuna taarifa za uwepo wimbi kubwa la watoto wa mitaani katika mji wa Nyamongo, huku maofisa wa maendeleo ya jamii wakitaka nguvu ya pamoja kukabiliana na tatizo hilo.

“Kuna wimbi kubwa la watoto wa mitaani hapa Nyamongo, hususan nyakati za usiku, na hii inaweza kuwa hatari hata kwa usalama,” Afisa Maendeleo ya Jamii katika vijiji vilivyo jirani na mgodi wa North Mara, Anthony Magoti amesema.

Magoti ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, amezitaka kamati za ulinzi katika ngazi mbalimbali kushirikiana kutatua tatizo la watoto wanaozagaa mitaani bila kwenda shule.

“Wazazi na walezi wanapaswa kuwajibika kila mtu katika nafasi yake kukabiliana na wimbi hili la watoto wa wanaozunguka katika mitaa hapa Nyamongo,” amesisitiza Magoti.Magoti akihutubia katika maadhimisho hayo

Magoti amesema baadhi ya watoto hao wanatoka katika vijiji vinavyozunguka mgodi wa North Mara na maeneo mengine, nje ya mgodi huo.

Inaelezwa pia kuwa hata kiwango cha utoro wa wanafunzi katika shule zilizo jirani na mgodi huo ambao pia unazungukwa na migodi wa wachimbaji wadogo, kinatisha.

“Utoro ni mwingi sana katika shule zetu hapa Nyamongo, jamii ielimishwe kuhusu umuhimu wa elimu,” amesema mwalimu wa shule za msingi katika vijiji vinavyopkana na mgodi huo, ambaye hakupenda kutajwa jina.


Tanzania huungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo hufanyika Juni 16 kila mwaka, huku yakiwa na kaulimbiu mbalimbali zenye lengo la kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi, ikiweo ya kupata elimu.

Kaulimbiu ya maandhimisho hayo mwaka huu inasema “Tutekeleze Ajenda 2040: kwa Afrika Inayolinda Haki za Watoto”.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages