NEWS

Monday 19 July 2021

Mwenyekiti CCM Mara, Namba Tatu amuunga mkono Mbunge Kembaki kuhusu upanuzi wa barabara Tarime Mjini
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye maarufu kwa jina la Namba Tatu (pichani juu) amejitokeza kuunga mkono msimamo wa Mbunge wa Tarime Mjini, Michael Kembaki kuhusu upanuzi wa barabara ya Nyamwaga kwa kiwango cha lami.

Namba Tatu ametumia nafasi hiyo pia kutoa onyo kwa watu wenye nia ovu ya kutaka kuhujumu mradi wa upanuzi wa barabara hiyo.

“Namuunga mkono Mbunge Kembaki, barabara ijengwe kama ilivyopangwa, na kila mbunge afanye kazi kwenye jimbo lake,” Nambatatu amesisitiza katika mazungumzo na Mara Online News mjini Tarime, jana.

Juzi, Mbunge Kembaki ametuma ujumbe mzito kwa mtu, au watu wanaotaka kuweka msukumo wa kuruka kilomita sita wakati wa upanuzi wa barabara ya Nyamwaga kwa kiwango cha lami.

Mbunge Kembaki

Akizungumza bila kumtaja mtu, katika mkutano wa hadhara mjini Tarime juzi, Kembaki amesema atasimama imara kuhakikisha barabara hiyo inapanuliwa kuanzia eneo la Jembe na Nyundo (Serengeti), bila kuhujumiwa.

“Tunahitaji barabara kwa maendeleo ya Tarime yetu, kuna kauli ilisemwa kwamba upanuzi wa barabara uanzie kule juu [eneo la Nyamwigura katika jimbo la Tarime Vijijini], naomba niwahakikishie, msimamo wangu na wa Serikali ni kwamba upanuzi utaanzia Jembe na Nyundo, ndio isonge kwenda kule, hapa haruki kitu,” amesisitiza Kembaki na kushangiliwa na umati mkubwa wa wananchi kuashiria kukubaliana na msimamo wake.

(Imeandikwa na Mara Online News)

1 comment:

  1. Safi sana wanaTarime mjini kwa kuligundua Hilo maana nilishangaa sana kitendo kile kiongoz anasema wataanzia Tarime vijijin aisee siasa sio kitu kizuri

    ReplyDelete

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages