NEWS

Monday 19 July 2021

TAWIRI yabuni mbinu za kuzuia tembo kuvamia mashamba vijijini




HATIMAYE Taasisi ya Utafiti wa Wanyampori Tanzania (TAWIRI) imebuni mbinu saba, ambazo tayari zimeanza kutumika kuzuia tembo kuvamia na kuharibu mashamba ya mazao ya chakula vijijini.

Akizungumza na Mara Online News mjini Mugumu wilayani Serengeti hivi karibuni, Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Uhusiano wa TAWIRI, Dkt Janemary Ntalwila ametaja mbinu hizo kuwa ni uzio wa pilipili wenye mchanganyiko wa tumbaku na mafuta ya kondoo, tofali za pilipili, tochi zenye mwanga mkali, honi mfano wa vuvuzela, mabomu ya machozi ya pilipili, fataki kubwa, uzio wa mizinga ya nyuki na wa kijiditali.

“Baadhi ya mbinu hizo zilikuwepo kwenye jamii lakini zilikuwa zimezoeleka kwa tembo, ikiwemo mwanga wa tochi, tumeamua kuziboresha ikiwemo kuja na tochi zenye mwanga mkali zaidi unaobadilika rangi, na mbinu mpya ya kupanga mizinga ya nyuki,” Dkt Janemary amesema.


Dkt Janemary akifafanua jambo katika mahojiano maalumu na Mara Online News

Amesema mbinu hizo za kuzuia tembo kuvamia mashamba ni rafiki na shirikishi, na kwamba TAWIRI imebuni mbinu hizo chini ya mpango mkakati wa kupunguza migongano baina ya binadamu na wanyamapori, ambao utekelezaji wake unaendelea katika maeneo mbalimbali nchini.

Mtafiti huyo amefanya mahojiano maalumu na Mara Online News muda mfupi baada ya kuwasilisha mada kuhusu mkakati ya kupunguza migongano baina ya binadamu na wanyamapori, kwenye warsha iliyofanyika mjini Mugumu, Serengeti mkoani Mara.

Amesema hadi sasa wanyamapori ni kivutio kikubwa cha utalii nchini na kusisitiza umuhimu wa kuwa na njia rafiki zitakazosaidia kupunguza migongano hiyo, zisizo za gharama kubwa kwa wananchi na zenye matokeo ya haraka.


Dkt Janemary akiwasilisha mada katika warsha hiyo

Katika mahojiano na Mara Online News, Dkt Janemary amesema wilaya ya Serengeti inaongoza kuwa na matukio ya migongano baina ya binadamu na wanyamapori, ikifuatiwa na wilaya ya Bunda, zote za mkoani Mara.

Kuhusu uharibifu wa mazao unaofanywa na wanyamapori waharibifu, amesema wilaya ya Serengeti inaongoza kitaifa, ikifuatiwa na Mvemero ya mkoani Morogoro.

Amesema TAWIRI inatekeleza mpango mkakati wa kupunguza migongano baina ya binadamu na wanyamapori kwa kushirikisha wadau wote muhimu, zikiwemo halmashauri za wilaya.

“Mdau wa kwanza ni halmashauri za wilaya, na mpango unahimiza wenye rasilimali kushiriki kwa asilimia 100,” Dkt Janemary amefafanua.

Mbali na halmashauri za wilaya, wadau wengine muhimu wanaoshiriki katika utekelezaji wa mpango mkakati huo ni Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Shirika la Uhifadhi la Kimataifa la Frankfurt Zoological Society (FZS), Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) na tasisi ya Honey Guide.


Wadau wakishiriki warsha hiyo ya kutafuta suluhisho la migongano baina ya binadamu na wanyamapori

Wakuu wa wilaya na viongozi wengine wa wilaya na chama tawala - CCM pia wanashirikishwa kikamilifu katika utekelezaji wa mpango huo, uliozinduliwa Oktoba 2020 na utekelezaji wake kuanza Aprili mwaka huu.

“Lengo la kwanza la mpango huu ni kushirikisha waathirika wenyewe [wananchi] kushiriki kikamilifu katika kubuni na kutekeleza mkakati huu,” Dkt Janemary amesema.

Amebainisha kuwa hadi sasa wilaya nane zimefikiwa na mpango huo, kati ya hizo, nne ni za mkoa wa Simiyu, mbili za Ruvuma na mbili nyingine za Kilimanjaro, na kwamba tayari makumi ya watu wamepata mafunzo kuhusu namna bora ya kutumia mbinu hizo mpya za kufukuza tembo kwa haraka.

Kwa mujibu wa Dkt Janemary, migongano baina ya binadamu na wanyamapori, imeongezeka katika miaka ya hivi karibuni, kwa sababu kuu tatu, ambazo ni mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la idadi watu na wanyamapori, wakiwemo tembo.


Tembo

“Ongezeko la binadamu ni sababu kubwa, lakini wanyama pia wameongezeka, na tatizo limeongezeka,” amesema Dkt Janemary.

Amesema kinachotakiwa ni wananchi kuzoea maisha ya kuishi na wanyamapori bila mingongano, kwani wanyamapori ni kuvutio kikubwa cha utalii nchini.

Kwa upande wake, Meneja Mradi wa FZS, Masegeri Rurai ametaja malengo ya warsha hiyo kuwa ni pamoja na kupitia mpango mkakati wa kitaifa wa kupunguza migongano baina ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu.

“Pia tunapeana uelewa wa pamoja juu ya migongano baina ya bindamu na wanyamapori wakali na waharibifu, na FZS inafanya nini kusaidia kupungunza tatizo,” Masegeri amesema katika warsha hiyo ya siku mbili, iliyoandaliwa na shirika hilo la FZS lenye makao makuu yake nchini Ujerumani.


Masegeri akiwasilisha mada

Akitoa mada katika warsha hiyo, Afisa Wanyamapori Mkuu kutoka Idara ya Wanyamapori - Wizara ya Maliasili na Utalii, Antonia Raphael amesisitiza umuhimu wa nguvu ya pamoja ya wadau katika kupunguza tatizo la migongano baina ya binadamu na wanyamapori.

Antonia amesema migongano hiyo ni miongoni mwa mambo yanayoinyima Serikali usingizi. “Kila siku Serikali inafikiri na kubuni mbinu kumaliza tatizo,” amesema.


Antonia akiwasilisha mada

Akizungumzia vifuta jasho na machozi, Antonia amesema kinachotolewa na Serikali si fidia, bali ni malipo ya kuwafariji waathirika wa wanyamapori wakali na waharibifu.

Kwa mantiki hiyo, Afisa Wanyamapori Mkuu huyo amesisitiza kuwa suluhisho la kudumu la migongano hiyo ni uanzishaji wa mpango wa matumizi ya ardhi katika vijiji vilivyopo maeneo hatarishi na kukomesha uingizaji mifugo kwenye makazi ya wanyamapori.

(Habari na picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages