NEWS

Wednesday 14 July 2021

RAS Mara awaonya watendaji wanaokaidi maelekezo ya wakubwa
KATIBU Tawala wa Mkoa (RAS) wa Mara, Albert Msovela (pichani juu) ametoa onyo kwa watendaji wa serikali mkoani humo wanaovunja na kukaidi maelekezo ya viongozi wa ngazi ya juu, ikiwemo kutohudhuria vikao vya kujadili shughuli za maendeleo.

RAS Msovela ametoa onyo hilo mjini Musoma jana, wakati akifungua kikao cha tathmini ya matokeo ya Mtihani wa Utimilifu (Mock), uliofanyika Juni 2 hadi 18, mwaka huu, ambapo matokeo yameonesha ufaulu umepanda kutoka asilimia 68.79 mwaka 2020, hadi asilimia 78.26 mwaka 2021.

Amesema moja ya sababu zinazokwamisha utendaji kazi, ni baadhi ya watendaji kuvunja itifaki kwa kutohudhuria vikao vya maelekezo na ushauri, akitolea mfano wa makatibu tawala wa wilaya walioshindwa kuhudhuria kikao hicho, kilichohudhuriwa na katibu tawala mmoja mkoa mzima.


Wajumbe kikaoni

Katibu Tawala huyo ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi, amemwaagiza Afisa Elimu wa Mkoa (REO) huo, Mwalimu Benjamin Oganga kusimamia itifaki kikamilifu kwa viongozi walio chini yake na kuhakikisha hatua kali za kinidhamu zinachukuliwa dhidi yao bila kuoneana haya.

Mapema akitoa tathmini hiyo, REO Oganga amesema Halmashauri ya Mji wa Bunda umeongoza kwa ufaulu katika mtihani huo, ikifuatiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, huku halmashauri za Tarime na Musoma Mji zikiwa za mwisho.

Amesema wanafunzi waliopata ufaulu wa daraja la kwanza hadi tatu, ni 5,350 (sawa na asilimia 23.85), waliopata daraja la nne ni 12,203 (sawa na asilimia 54.42), huku jumla ya wanafunzi waliopata daraja la nne na daraja sifuri wakiwa 16,077, sawa na asilimia 76.15 ya wanafunzi wote 22,535 waliofanya mtihani huo.


Kikao kinaendeleo

REO huyo amesema ufaulu katika masomo ya Kiswahili, Uraia, Kemia na Kiingereza ulikuwa mzuri na kwamba jitihada zaidi zinahitajika kwa masomo ya Hisabati, Baiolojia, Jiografia, Historia na Fizikia.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa elimu wamependekeza baadhi ya hatua zinazotakiwa kuchukuliwa ili kukuza ufaulu, ikiwa ni pamoja na kuimarisha uhusiano kati ya walimu na wazazi, kuwa na huduma ya chakula kwa wanafunzi shuleni, nidhamu kwa walimu na wanafunzi, usahihishaji wa kazi za watoto, uwajibikaji, ufuatiliaji na ukaguzi wa masomo.


Umakini kikaoni

Mapendekezo mengine ni utatuzi wa kero za walimu, kutoa motisha, uimarishaji vitendea kazi kwa walimu na uongezaji vyumba vya madarasa.

Wajumbe wajumbe tathmini hiyo walikuwa walimu, wathibiti ubora wa shule, Chama cha Walimu Tanznaia (CWT) Mkoa wa Mara, Tume ya Utumishi ya Walimu (TSC), Sekretarieti ya Mkoa, makatibu tawala, wakurugenzi na maafisa elimu wa wilaya.

(Imeandikwa na Maximillian Ngessi, Musoma)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages