NEWS

Tuesday 31 August 2021

Maelfu ya wananchi mji wa Mugumu waanza kunufaika na mradi wa majisafi wa Manchira
HATIMAYE wakazi wa mji wa Mugumu na vijiji vilivyo jirani wilayani Serengeti, mkoa wa Mara wameanza kupata huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza, baada ya Serikali ya awamu ya sita kukamilisha ujenzi wa Chujio la maji katika bwawa la Manchira, nje kidogo ya mji huo.

Mradi wa ujenzi wa chujio hilo ambao umegharimu Sh milioni 947, ulikamilika na kuzinduliwa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, hivi karibuni.

“Furaha yangu ni kuona wananchi wanapata majisafi, na dhamira ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan ni kumtua mama ndoo kichwani,” Waziri Aweso amesema wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa National uliopo mjini Mugumu.


Waziri Aweso (kulia aliyevaa skafu) na viongozi mbalimbali akishuhudia bomba likitoa maji kutoka bwawa la Manchira wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi huo kwenye uwanja wa National mjini Mugumu.

Kwa mujibu wa waziri huyo, ujenzi wa chujio la maradi wa maji wa Manchira ulikuwa miongoni mwa miradi ya maji kichefuchefu (iliyochukua muda mrefu), iliyowashinda wakandarasi wengi kwa muda mrefu, hata baada ya kuigharimu Serikali mamilioni ya fedha.

Hata hivyo, mwishoni mwa mwaka jana 2020, Waziri Aweso aliamua kukabidhi ujenzi wa chujio hilo kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA), chini ya Mkurugenzi Mtendaji wake kwa kipindi hicho, CPA Joyce Msiru, kazi ambayo mamlaka hiyo imefanikiwa na kuukwamua mradi.

“Mradi huu ilikuwa kila mtu anayeutekeleza unamshinda, nimeweka vidume kweli kweli vimeshindwa. Lakini kwa CPA Msiru mradi huu haukuwa mgumu, ulikuwa mlaini kama biskuti, ameumumunya,” Waziri Aweso amesema.


Waziri Aweso (mbele) na CPA Msiru wakikagua miundombinu ya mradi wa maji wa Manchira

Viongozi na wananchi wamepokea kwa furaha kukamilika kwa mradi huo na kuhudhuria uzinduzi wake, wakimimina pongezi kwa MUWASA, Waziri Aweso na Serikali kwa ujumla, kwa kuwezesha utatuzi wa kero ya majisafi iliyowakabili katika mji wa Mugumu.

“Utendaji wako [Waziri Aweso] unadhihirisha kwamba Rais hakukosea kukuamini na kukupatia nafasi hiyo. Unaitendea haki Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),” Katibu wa CCM Mkoa wa Mara, Shaibu Ngatiche amesema.


Kwaya ya Wizara ya Mji ikitumbuiza katika hafla ya uzinduzi huo

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Serengeti, Jacob Begha amempongeza waziri huyo kwa namna alivyofuatilia na kuhakikisha mradi wa maji wa Manchira unakamilika na kuwezesha wakazi wa Mugumu kupata majisafi.

“Juhudi zako Waziri zinaonesha una kusudi jema kwa wananchi mkoa wa Mara. Unajituma sana kuipa heshima Serikali na nchi yetu. Tunakushukuru kwa kutuzindulia mradi huu, kwani huduma ya majisafi ni muhimu kwa wakazi wa mji wa Mugumu unaokua kwa kasi,” Begha amesema.


Waziri Aweso (kulia) akicheza na kiongozi wa kwaya wakati Kwaya ya Wizara ya Maji ikiimba wimbo maalumu katika uzinduzi huo.

Naye Mbunge wa Serengeti, Amsabi Mrim amesema “Kukamilika kwa mradi huu kumeleta matumaini makubwa kwa wananchi wa Mugumu. Mradi huu utatuletea heshima, kwani mji huu unaelekea kuwa wa kitalii.”

Hata hivyo, mbunge huyo amesema bado wananchi katika maeneo mengi ya jimbo hilo wanakabiliwa na uhaba wa majisafi. Hivyo aliiomba Serikali kupitia kwa Waziri Aweso, kuendelea kutenga bajeti ya uboreshaji na upatikanaji wa huduma ya majisafi.

Mkazi wa mjini Mugumu, Consolata Mayunga anaishukuru Serikali kwa kutekeleza mradi huo kwa mafanikio, akisema hatua hiyo imedhihirisha wazi dhamira ya dhati ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani, bila kujali itikadi yake.

Mkazi mwingine wa mji huo, Butariani Marwa anasema “Sasa vita vya ndani na migongano kwa wanandoa vilivyokuwa vinasababishwa na tatizo la maji vimeisha. Sasa hivi kero ya maji imeisha, wanamama wanapika, hatuna wasiwasi.”


Waziri Aweso (katikati) akisoma maelezo ya jiwe la uzinduzi alioufanya katika chujio la mradi wa maji wa Manchira

Katika taarifa yake, CPA Msiru ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Idara ya Usambazaji Majisafi na Usafi wa Mazingira, Wizara ya Maji, amesema MUWASA ilianza kutekeleza mradi huo mwezi Oktoba 2020 kwa kutumia wataalamu wa ndani na kukamilisha utekelezaji kwa asilimia 100, ndani ya kipindi cha miezi saba.

“Mradi huu wa bwawa la maji la Manchira, unaweza kutumika pia kama kivutio kwa watalii,” CPA Msiru ameongeza na kuwahimiza wananchi kulinda miundombinu ya mradi huo, ili udumu muda mrefu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mugumu (MUGUWASA), Hussein Nyemba amemweleza Waziri Aweso kwamba, kwa sasa watu 39,045 wanapata majisafi ya bomba kutoka mradi huo wa Manchira.

Nyemba amebainisha kuwa mradi huo una uwezo wa kuzalisha lita za ujazo 1,860 kwa siku na kwamba baada ya ujenzi wa chujio kukamilika, mapato ya MUGUWASA yameongezeka kutoka Sh milioni 12 hadi milioni 17 kwa mwezi.

“Kwa sasa tuna wateja 2,083 waliounganishiwa huduma ya maji ya bomba na wananchi wengine wengi wanahitaji kuunganishiwa huduma hii,” amesema.


MsirWaziri Aweso (wa tatu kushoto mbele), CPA Msiru (wa pili kushoto), Mbunge wa Serengeti, Amsabi Mrimi (wa nne kushoto), Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Serengeti, Jacob Begha (wa tano kushoto) na viongozi mbalimbali wakiwasili kukagua mradi wa chujio la maji la mradi wa Manchira, kabla ya hafla ya uzinduzi.

Waziri Aweso amehitimisha hotuba yake ya uzinduzi wa mradi huo, kwa kuitaka MUGUWASA kuhakikisha inatoa huduma bora na inayokidhi mahitaji kwa wananchi katika mji wa Mugumu na vijiji jirani.

Ametumia nafasi hiyo pia kuwataka wataalamu kuepuka vitendo vya ubadhirifu wa fedha za miradi ya maji na kutoa bili zisizoakisi matumizi wananchi bili za maji.

“Wananchi wasipewe bili zisizoakisi matumizi yao kuhusu bili za maji. Pamoja na hilo, wale watakaochezea pesa ya mama Samia [inayoidhinishwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kugharimia utekelezaji wa miradi ya maji] wataishia jela,” Waziri Aweso ameonya.

Sehemu ya miundombinu ya chujio la maji katika mradi wa Manchira

Kwa ujumla, maji ni rasilimali inayogusa ustawi na maisha ya kila kiumbe hai, ikiwemo binadamu, wanyama, mimea na mazingira.

Aidha, maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kiasi kikubwa yanategemea uwepo wa huduma endelevu ya majisafi na salama na ya kutosha. Kwa maneno mengine, maji ni injini ya uchumi.

Dira ya Maendeleo ya Taifa (Tanzania Development Vision – TDV 2025) pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020 imebainisha kuwa maji ni miongoni mwa vipaumbele katika kukuza uchumi.

Kuwekwa kwa maji kama kipaumbele ni kutokana na mchango wake katika uzalishaji wa umeme, kilimo cha umwagiliaji, ufugaji, viwanda, usafirishaji na uchukuzi; lakini pia kupunguza magonjwa ya milipuko, hivyo kupunguza umaskini.

Serikali inaendelea kuweka mikakati mbalimbali kwa ajili ya kufikia Malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, kupitia utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP 2006 - 2025).

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages