NEWS

Tuesday 3 August 2021

Mnada wa mifugo Magena uliotangazwa kwa ‘mbwembwe’ wakwama kufunguliwa
MNADA wa Kimataifa wa Mifugo Magena uliotangazwa kuruhusiwa na Waziri wa Maendeleo ya Mifungo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, baada ya kufungwa kwa miaka zaidi ya 20 iliyopita, umekwama kufunguliwa Julai 22, mwaka huu - kama Halmashauri ya Mji wa Tarime ilivyokuwa imeutangazia umma.

Katika ziara yake wilayani Tarime Juni 12, mwaka huu, Waziri Ndaki alitembelea eneo la Magena na kuiagiza halmashauri hiyo kutangaza siku rasmi ya mnada huo, ambapo baadaye ilitangaza kwamba utakuwa unafanyika kila Alhamisi.

“Utazinduliwa Julai 22, 2021, ninavyozungumza na wewe tingatinga lipo eneo la mnada linachonga barabara za kuingia na kutoka mnadani hapo, wakati huo maofisa ardhi nao wapo eneo hilo wakichora ramani namna vibada vitakavyokaa,” Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Daniel Komote aliiambia Mara Online News, siku chache baada ya agizo la Waziri Ndaki.
Waziri Ndaki (katikati) siku alipotembelea eneo la mnada wa Magena, nje kidogo ya mji wa Tarime. Kulia ni Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara na kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Daniel Komote.

Hata hivyo, wakizungumza na Mara Online News wilayani Tarime juzi, wakazi wa mtaa wa Magena, wameeleza kushangazwa na namna suala la ufunguzi wa mnada huo linavyoshughulikiwa kisiasa.

“Sisi wananchi wa Magena tunaomba mnada huo ufunguliwe, tumechoka na ahadi za wanasiasa wakati tunakosa fursa za biashara na mapato ya ng’ombe wanaochepushwa kwenda nchi jirani yanapotea,” Justin Manga amesema.

Wananchi wengine wamehoji inakuwaje mnada mkubwa kama huo, ushindwe kufunguliwa kutokana na ukosefu wa miundombinu muhimu kama vile ofisi na vyoo, wakati utakuwa chanzo muhimu cha mapato ya halamshauri hiyo.

“Hiyo haingii akilini, labda halmashauri yetu haina wachumi wazuri, kwani kwa mfano kama wangetangaza kubinafsisha choo wangepata mwekezaji haraka, na gharama nyingine za mnada zingepatikana kwa kugawa viwanja vya biashara kama vile hoteli na mitumba,” Timothy Itembe amesema.

Waziri Ndaki (kushoto) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Magena kuhusu ruhusa ya kufunguliwa kwa mnada wa Magena. Kulia ni Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini.

Mara Online News imewasiliana na viongozi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, akiwemo Mwenyekiti Komote ili kujua kilichokwamisha ufunguzi wa mnada huo, lakini hawakuwa tayari kuzungumzia suala hilo.

(Imeandikwa na Mobini Sarya, Tarime)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages