NEWS

Friday 20 August 2021

Wasanii Tanzania kunufaika na Itifaki ya Usajili na UlinziWASANII wa Tanzania wanatarajiwa kuanza kunufaika na Itifaki ya Usajili na Ulinzi wa Hiari ya Haki Miliki, baada ya nchi wanachama wa Shirika la Kanda ya Afrika la Miliki Ubunifu (ARIPO) kuipitisha.

Tayari wanachama wa ARIPO wameanza kukutana nchini Uganda leo kujadili masuala ya Miliki Bunifu Kanda ya Afrika.

Mkutano huo mkuu wa siku tisa uliofunguliwa na Mwanasheria Mkuu wa Uganda, Kiryowa Kiwanuka, unafanyika katika hoteli ya Munyonyo jijini Kampala.

Kiwanuka amesisitiza ushiriki wa nchi wanachama kujadili kwa kina itifaki hiyo, ili iongeze tija na ufanisi kwa nchi katika kulinda wasanii na kazi zao.

Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) nchini Tanzania, Godfrey Nyaisa ambaye anashiriki mkutano huo, amesema washiriki watajadili na kupitisha Itifaki ya Usajili na Ulinzi wa Hiari wa Haki Miliki kama itaridhiwa na mawaziri wa nchi wanachama.

“Kwa nchi ya Tanzania, utiaji saini wa Itifaki hii itasaidia wasanii kusajili na kupata ulinzi wa kazi zao nje ya nchi wanachama, tofauti na ilivyo sasa ambapo msanii akisajili ARIPO anaweza kuomba ulinzi nchi mbalimbali,” CEO Nyaisa amesema.


CEO Nyaisa (kushoto) akishiriki mkutano huo

CEO huyo wa BRELA ameongeza kuwa Itifaki hiyo ya Usajili na Ulinzi wa Hiari ya Miliki Bunifu itasainiwa na mawaziri wa nchi wanachama wa ARIPO Agosti 27 na 28, 2021 baada ya kuijadili kwa kina.

BRELA ni taasisi inayosimamia masuala ya Miliki Ubunifu ambayo ni nyanja inayohusu uwezo wa ubunifu wa mtu au watu katika kuunda vitu au kutoa huduma.

Inahusisha masuala ya hataza, tunzi, fasihi na kazi za sanaa, alama kwenye bidhaa na huduma, maumbo ya mikebe ya bidhaa na nyinginezo.

Pia inahusu uwezo wa ubunifu wa binadamu unaotambuliwa chini ya mfumo wa Sheria wa Ulinzi wa Bunifu mbalimbali.

Mbali ya ushiriki wa BRELA, washiriki wengine kutoka Tanzania ni Wizara ya Viwanda na Biashara na Chama cha Haki Miliki Tanzania (COSOTA).

MaraOnlineNews-Updates

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages