NEWS

Friday 20 August 2021

KUBATA yaja na dhamira ya kukuza uchumi kupitia kilimo, ufugaji




KAMPUNI ya Kukuza Uchumi na Kuboresha Afya Tanzania (KUBATA PLC) itazinduliwa Agosti 26, 2021, Mkurugenzi Mkuu (DG), Chacha Marwa Getamuru amethibitisha.

“Uzinduzi utafanyika kwenye ukumbi wa Blue Sky mjini Tarime, kuanzia saa nane mchana,” DG Getamuru ameiambia Mara mjini Tarime, hivi karibuni.

Amebainisha kuwa uzinduzi huo utahusisha utambulisho wa KUBATA PLC na semina ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kuwekeza katika kampuni hiyo.

“Kamupni hii itakuwa inajihusisha na shughuli za kilimo cha mazao, ufugaji wa aina zote, viwanda vidogovidogo na masoko, lakini pia kuzalisha bidhaa kutokana na mazao ya kilimo na ufugaji,” amefafanua.

Ameongeza “Dira ya KUBATA ni kuwa kampuni inayoongoza kutoa huduma imara kwa haki na kuwezesha ukuaji wa uchumi kwa kila mtu, na dhima yetu ni kukuza uchumi na kuboresha afya kwa kutumia kilimo, ufugaji, viwanda, Saccos na rasilimali watu.”


DG Getamuru akizungumza na Mara Online News

DG Getamuru amesema KUBATA PLC imejengwa katika misingi mikuu sita, ambayo ni muhimu kwa kila mwanachama wake kuitekeleza na kuizingatia wakati wote awapo ndani na nje ya kampuni hiyo.

Ametaja misingi hiyo kuwa ni haki na usawa, ubunifu, uthubutu, bidii, umoja na uduma bora.

“Huduma kuu za KUBATA PLC ni kilimo, ufugaji, viwanda, masoko, mikopo, Saccos, bima ya afya, uchimbaji wa mabwawa na visima,” DG Getamuru amesema.

Ameongeza kuwa kampuni hiyo imejikita katika bidhaa za chakula, kama vile nafaka (mchele, sembe, dona, unga wa lishe na ngano), mboga (maharage, samaki, dagaa na mboga za majani), viungo (mafuta ya alizeti, chai mbadala, nyanya, vitunguu, karanga, mchaichai, chumvi na sukari) na matunda (ndizi, nanasi, parachichi, machungwa, mapapai, matikiti na matango).

“Bidhaa nyingine ni vinywaji (maji, maziwa na juisi mbalimbali), viazi (viazi vitamu na viazi ulaya), mihogo (unga wa udaga), miwa (ya sukari na juisi), ndizi (za kupika na kutengeneza biskuti na ufugaji (ng’ombe, mbuzi, kondoo, kuku, nyuki, samaki, bata n.k,” DG Getamuru ameongeza.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages