NEWS

Monday 23 August 2021

Mageuzi sekta ya maji: Wananchi Shirati wafurahi kurejeshewa huduma, waishukuru SerikaliBAADA ya dhiki ni faraja. Ndivyo tunavyoweza kuielezea furaha ya maelfu ya wakazi wa mji mdogo wa Shirati wilayani Rorya, baada ya kurejeshewa huduma ya majisafi ya bomba kutoka Ziwa Victoria, waliyoikosa kwa miaka sita.

Wananchi hao licha ya kuwa jirani na watunzaji wa rasilimali maji ya ziwa hilo, walikosa huduma hiyo tangu mwaka 2015, kutokana na ubovu wa miundombinu ya mradi wa maji wa Shirati.

Hata hivyo, wataalamu wa Serikali kupitia Wizara ya Maji na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA), wamefanikiwa kuhuisha mradi huo, baada ya kukamilisha ukarabati wa miundombinu yake kwa asilimia 100.


Wakazi wa Shirati wamerejeshewa huduma ya maji ya bomba

Hivi karibuni, Mara Online News imezungumza na baadhi ya wakazi wa mji wa Shirati kwa nyakati tofauti, kuhusu namna walivyoanza kunufaika na mradi huo.

“Tunaishukuru sana Serikali yetu kwa kutoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya mradi wa maji ya bomba, iliyokuwa imeharibika na kutukosesha maji kwa miaka sita. Sasa hivi wana-Shirati tunapata majisafi kama zamani, ni faraja kubwa sana,” Mkazi wa Shirati, Stela Otieno anasema.

Mkazi mwingine wa mji huo, Monica Tisa anasema “Kero yetu kubwa ilikuwa maji, sasa tunapata huduma ya majisafi ya bomba, tunamshukuu sana Rais wetu Samia Suluhu Hassan na wote waliohusika katika kuturejeshea huduma hii muhimu, Mungu awabariki.”

Mussa Okello ni mkazi wa Shirati pia. Anasema “Ufufuaji wa mradi huu wa maji umepunguza kwa asilimia kubwa ugomvi na migogoro ya ndoa miongoni mwa wananchi wa Shirati, kwa sababu wanawake walikuwa wanaondoka alfajiri kwenda kutafuta maji na kuchelewa kurudi nyumbani.”


Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi (mwenye kofia) akimtwisha mkazi wa Shirati ndoo yenye maji ya bomba mjini Shirati, hivi karibuni. Anayepiga makofi ni Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA wa kipindi hicho, CPA Joyce Msiru ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Idara ya Usambazaji Majisafi na Usafi wa Mazingira, Wizara ya Maji.

Chimbuko la urejeshaji huduma ya maji ya bomba katika mji wa Shirati limetokana na kazi za Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (Mb) na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (Mb), waliofanya ziara kwa nyakati tofauti katika mji huo wenye wakazi 30,804, kulingana na sesa ya watu na makazi ya mwaka 2012.

Januari 6, mwaka huu, Waziri Aweso alizuru Shirati, ambapo katika kutekeleza agizo la Waziri Mkuu Majaliwa, aliiagiza MUWASA kukarabati miundombinu ya mradi huo wa maji, ili kurejesha huduma kwa wananchi kama ilivyokuwa awali.

Siku hiyo hiyo, Waziri Aweso aliahidi kuipatia MUWASA Sh milioni 247 kwa ajili ya kuanza ukarabati wa miundombinu hiyo, ahadi ambayo ilitekelezwa Januari 27, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA wa kipindi hicho, CPA Joyce Msiru, ukarabati wa miundombinu ya mradi huo ulianza baada ya ofisi yake kupokea fedha kutoka serikalini.

CPA Msiru anasema MUWASA imekamilisha utekelezaji wa mradi huo kwa asilimia 100, kwa gharama ya Sh milioni 493 zilizotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Maji.


Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi (mwenye kofia) akimpongeza CPA Joyce Msiru (wa pili kushoto), kwa kazi nzuri ya uhuishaji mradi wa maji wa Shirati, alipokwenda kuukagua, hivi karibuni. Kulia ni mkazi wa mji huo akifurahia huduma ya maji.

CPA Msiru anasema ukarabati ulihusisha kazi mbalimbali, ikiwemo marekebisho ya mashine ya kusukuma maji (pump) katika kituo cha Michire (yenye uwezo wa kusukuma maji kwa mita za ujazo 21 kwa saa) na nyingine yenye uwezo wa kusukuma maji kwa mita za ujazo 90 kwa saa.

Pia, marekebisho makubwa ya mabomba katika njia kuu ya kusafirisha maji kutoka kituo cha kusukuma maji cha Michire mpaka kwenye tenki la kuhifadhi maji lililopo katika kilele cha mlima Obhoke, kwa urefu wa kilomita tano.

“Katika urefu huo, mabomba mapya yenye kipenyo cha milimita 200 yalilazwa kwa urefu wa mita 1,330. Ukarabati mwingine ni wa tenki la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita 1,500,000 lililopo eneo la mlima Obhoke na mfumo wa usambazaji maji kwa kuweka bomba mpya kwa urefu wa kilomita saba,” CPA Msiru anaongeza.

Anasema hadi sasa wateja 602, wakiwemo 567 wa majumbani, sawa na wastani wa wakazi 5,000 wa mji wa Shirati, wanapata huduma ya maji ya bomba, kupitia tenki lenye ukubwa wa mita za ujazo 1,500.

CPA Msiru anasema MUWASA inaendelea kupokea maombi kutoka kwa wakazi wa vijiji vya Obwere, Michire, Obhoke, Ngasaro na Kabwana wanaohitaji kuunganishiwa huduma ya maji ya bomba katika makazi yao.

Anabainisha kuwa gharama za kuunganisha huduma ya maji ya mradi huo katika mji wa Shirati ni kati ya Sh 11,500 na 250,000 (kutegemea na umbali wa eneo la mteja kutoka bomba la kusambaza majisafi).


Meneja Ufundi wa MUWASA wa kipindi hicho, Nicas Mugisha ambaye kwa sasa ni Kaimu MD wa Mamlaka hiyo, akimwonesha RC Hapi (katikati) chanzo cha mradi wa maji wa Shirati katika Ziwa Victoria. Kushoto ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye maarufu kwa jina la Namba Tatu

Mradi wa maji wa Shirati umeendelea kutembelewa na viongozi mbalimbali, kuanzia wakati wa ukarabati hadi kukamilika kwake, wakiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (Mb).

Agosti 13, mwaka huu, Waziri Aweso alikwenda kuzindua ukarabati wa miundombinu ya maji unaotekelezwa na MUWASA katika mji wa Shirati.

Katika hotuba yake kwa mamia ya wananchi kwenye uwanja wa Obwere mjini Shirati, Waziri huyo aliipongeza MUWASA, chini ya uongozi wa CPA Msiru kwa kazi nzuri ya kuhuisha mradi na kuwarejeshea wakazi wa mji huo huduma ya majisafi.

“Furaha yangu ni kuona wananchi wanapata majisafi, na dhamira ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan ni kumtua mama ndoo kichwani,” alisema Waziri Aweso.

Waziri wa Maji Jumaa Aweso akiwa amejitwisha ndoo yenye maji, wakati alipokwenda kuzindua ukarabati wa miundombinu ya mradi wa maji katika mji wa Shirati. Kulia ni Mbunge wa Rorya, Jafari Chege.

Waziri huyo alitumia wasaa huo pia kumteua CPA Msiru kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Usambazaji Majisafi na Usafi wa Mazingira, Wizara ya Maji, na kesho yake alimteua Meneja Ufundi wa MUWASA, Nicas Mugisha kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo.

“Dada yangu na Mkurugenzi, umeweza kuniheshimisha, kulikuwa na miradi kichefuchefu ambayo utekelezaji wake ulikuwa ni mgumu, mradi wa kwanza ni Mugumu [mradi wa maji wa Manchira wilayani Serengeti], kila mtu ambaye anautekeleza unamshinda, nimeweka vidume kweli kweli vimeshindwa.

“Lakini huyu mama nilivyomwambia nenda kautekeleze ule mradi, kwake ulikuwa siyo mgumu. Lakini pia tumempa miradi mingi, tumempa huu mradi wa Shirati, tulimpa siku 30, yeye amefanya kwa siku 21. Nani kama Joyce ndugu zangu? Huyu mama tumempa kazi ngumu, kila kazi tuliyompa ameweza kuikwamua.

“Kwa mamlaka niliyopewa na kuaminiwa na Rais wangu Samia Suluhu Hassan, ndugu yangu Joyce Msiru ninamteua kuwa Mkurugenzi wa mamlaka za maji zote nchini, kwa sababu hii kazi anaiweza,” Waziri Aweso alisema na kushangiliwa na wananchi mkutanoni hapo.


Waziri wa Maji Jumaa Aweso (kushoto) akimpongeza CPA Joyce Msiru (kulia) mbele ya wananchi katika uwanja wa Obwere mjini Shirati, wakati wa hafla ya uzinduzi huo.

Akizungumzia uhuishaji wa mradi wa maji wa Shirati, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Maji, Florence Temba alisema “Mradi huu ni mafanikio ya kihistoria kwa wananchi wa Shirati, ikiwa ni utatuzi wa changamoto kubwa ya maji iliyowakabili kwa muda mrefu.”

Miongoni mwa viongozi waliofuatana na Waziri Aweso katika ziara hiyo ya Shirati, ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Shaibu Ngatiche.

Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka na Mbunge wa Rorya, Jafari Chege, ambao kwa nyakati tofauti katika hafla hiyo, waliishukuru Serikali na kuhimiza wananchi kulinda na kutunza miundombinu ya mradi wa maji katika mji wa Shirati, ili uwe endelevu, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo, kwa sababu huduma ya majisafi haina mbadala na idadi ya watu na matumizi vinaongezeka.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages