NEWS

Thursday 9 September 2021

Makuruma ahimiza tahadhari dhidi ya Korona wilayani Serengeti




MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Ayub Mwita Makuruma (pichani juu) amehimiza madiwani na watendaji kusaidia kuelekeza wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO 19).

Makuruma amesisitiza hilo wakati akifungua kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo mjini Mugumu, kilichohutubiwa na Mkuu wa Wilaya, Dkt Vicent Mashinji jana Septemba 8, 2021.


Dkt Mashinji akihutubia kikao hicho

“Ni muhimu sana tuendelee kuchukua tahadhari kwa sababu korona bado ipo, tuelekeze wananchi wetu kuchukua tahadhari, ikiwemo kutumia vitakasa mikono na maji tiririka kunawa mikono mara kwa mara.

“Lakini pia tuendelee kumwomba Mungu aweze kutukomeshea hayo maradhi,” Makuruma amesisitiza.

Kwa mujibu wa Makuruma ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Busawe, mlipuko wa Korona umeiathiri halmashauri pia katika mapato, kwani kwa sehemu kubwa inategemea utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Mwenyekiti huyo ametumia nafasi hiyo pia kuwahimiza madiwani na wataalamu wa halmashauri hiyo kuwa na michango inayochochea ufanisi katika miradi ya maendeleo ya wananchi.


Madiwani kikaoni

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Kivuma Hamisi Msangi na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa wilaya hiyo, Jacob Begha, miongoni mwa viongozi wengine.

(Habari na picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages