NEWS

Thursday 9 September 2021

Mradi wa miji 28 kufuta kilio cha maji Tarime, Rorya
KILIO cha maji cha muda mrefu kwa wananchi wa wilaya za Tarime na Rorya mkoani Mara kinatarajiwa kufikia ukomo, baada ya Serikali ya Tanzania kupokea Dola za Marekani milioni 500, kwa ajili ya kugharimia utekelezaji miradi ya kimkakati katika miji 28 nchini.

Mradi huo uliopewa jina la Mradi wa Maji wa Miji 28 utawawezesha maelfu ya wananchi wa Tarime na Rorya kupata huduma ya majisafi ya uhakika kutoka Ziwa Victoria.

Fedha za kugharimia utekelezaji wa mradi huo ambazo ni sawa na Shilingi za Tanzania zaidi ya trilioni moja, ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya India, kupitia Benki ya Exim India.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amewambia waandishi wa habari jijini Dodoma leo Septemba 9, 2021 kwamba tayari maandalizi ya kutekeleza miradi hiyo yameanza.

“Dhamira ya Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ni kumtua Mama ndoo ya maji kichwani. Tunamshukuru sana kwa kuendelea kutupatia fedha nyingi.

“Hivi karibuni ametuongeza fedha nyingine kiasi cha shilingi bilioni 207 mbali na fedha iliyoidhinishwa na Bunge la Bajeti 2020/2021 kiasi cha shilingi bilioni 680,” Waziri Aweso amesema.

Alikuwa akizungumza katika kikao na wanahabari kilicholenga kuonesha mageuzi makubwa yaliyofanywa na yanayoendelea katika sekta ya maji, lakini pia kutambua mchango wa vyombo vya habari katika kuufahanisha umma maendeleo yanayofanywa na Serikali.


Waziri Aweso akizungumza na wanahabari

Ukiweka kando Tarime na Rorya, miji mingine itakayonufaika na mradi huo ni Korogwe, Muheza, Pangani, Wanging’ombe, Makambako, Kayanga, Njombe, Manyoni, Nanyumbu, Sikonge na Chunya.

Mingine ni Kasulu, Kilwa, Lujewa, Mugumu, Geita, Chato, Singida Mjini, Kiomboi, Mpanda, Chemba, Urambo, Ifakara, Chamwino, Mafinga, Makonde Plateau na Songea.


Kikao kikiendelea

Aidha, Waziri Aweso alizungumzia miradi ya maji vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini na Mijini (RUWASA), amebainisha kuwa shilingi zaidi ya bilioni 450 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza mikataba katika miradi 1,176 ili kuongeza upatikanaji maji vijijini, kutoka asilimia 72.3 ya sasa hadi asilimia 77 ifikapo mwaka 2022.

“Lengo la Serikali ni kwamba ifikapo mwaka 2025 maeneo ya vijijini hali ya upatikanaji wa huduma ya maji iwe imefikia asilimia 85 na mwelekeo ni mzuri,” amesema.

Ameongeza kuwa wakati RUWASA inaanzishwa mwaka 2019 ilirithi miradi 177 kutoka Halmashauri mbalimbali nchini na kwamba hadi sasa miradi 115 imekamilika na 62 inatarajiwa kukamilika Desemba 2021.

(Na Mwandishi wa Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages