NEWS

Friday 10 September 2021

Maadhimisho Siku ya Mara: RAS aalika wadau wa maendeleo kushiriki




WANANCHI, wakiwemo wafanyakazi, wajasiriamali na wadau wote wa maendeleo ndani na nje ya mkoa wa Mara, wanaalikwa kushiriki maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara, yatakayofanyika Septemba 13 - 15, 2021 katika Chuo cha Ualimu Tarime.

Mwaliko huo umetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) wa Mara, Albert Msovela, kupitia mkutano maalum na waandishi wa habari mjini Musoma, leo Septemba 10, 2021.

Maadhimisho haya huendeshwa na nchi za Kenya na Tanzania, chini ya uratibu wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) yenye makao yake makuu Kisumu, Kenya.


RAS Msovela akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)

“Madhimisho ya Siku ya Mara ni utekelezaji wa maazimio ya mkutano wa 10 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Bonde la Ziwa Victoria, uliofanyika Mei 4, 2012 Kigali nchini Rwanda, ambao ulielekeza kuwa maadhimisho ya Siku ya Mara yawe yanafanyika Septemba 15 kila mwaka, kuanzia mwaka 2012.

“Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Mara mwaka huu inasema “TUHIFADHI MTO MARA KWA UTALII NA UCHUMI ENDELEVU,” RAS Msovela amesema.

Amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuongeza msukumo wa kuhifadhi Bonde la Mto Mara na kuendelea kutangaza na kufuatilia tukio muhimu la nyumbu wanaovuka mto huo katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Tanzania kuelekea Mbuga ya Maasai-Mara, Kenya.


Nyumbu wakivuka Mto Mara katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Tanzania.

RAS Msovela amesema maadhimisho hayo yataambatana na shughuli mbalimbali, zikiwemo za uzinduzi wa kampeni ya mkoa ya kupanda miti rafiki kwa vyanzo vya maji na mazingira, na uwekaji vigingi kwenye mipaka ya hifadhi ya Mto Mara katika vijiji vya Mrito na Kerende.

Kwa mujibu wa RAS huyo, miti zaidi ya 10,000 inatarajiwa kupandwa na vigingi 60 vitasimikwa katika maeneo hayo.



Ametaja shughuli nyingine kuwa ni maonesho ya uhifadhi na ujasiriamali kutoka taasisi za umma na za kijamii ndani na nje ya mkoa wa Mara na michezo mbalimbali inayohamasisha jamii kutunza na kuhifadhi Mto Mara na bonde lake, hususan katika vijiji vinavyopakana na mto huo.

“Nitoe mwaliko kwa wananchi wa mkoa wa Mara, wafanyakazi, wajasiriamali na wadau wote wa maendeleo ndani na nje ya mkoa, kushiriki maadhimisho haya yatakayofanyika katika viwanja vya Chuo cha Ualimu Tarime,” RAS Msovela amesisitiza.

Mto Mara unaanzia katika chemchem ya Enapuyapui kwenye misitu ya milima ya Mau ambapo maji ya mto huo hutiririka kupitia Mbuga ya Maasai-Mara, Kenya na hatimaye katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti Tanzania, kabla ya kumwaga maji yake katika Ziwa Victoria.


Sehemu ya Mto Mara


Sehemu ya milima ya Mau

Eneo la Bonde la Mto Mara lina ukubwa wa kilomita za mraba 13,325, huku mto wenyewe ukiwa na urefu wa kilomita 400.

Nchi ya Tanzania inamiliki asilimia 35, huku Kenya ikimiliki asilimia 65 ya eneo lote la Bonde la Mto Mara.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages