NEWS

Monday 6 September 2021

Mashindano ya Serengeti Migration Marathon yalivyofana




MAMIA ya wadau na wanariadha kutoka mikoa mbalimbali Tanzania na Kenya wamejitokeza kushiriki mashindano ya siku mbili ya Serengeti Migration Marathon 2021 wilayani Serengeti, Mara.

Mashindano hayo yamefanyika mjini Mugumu juzi na Fort Ikoma jana, yakihusisha mbio za kilomita 42, 21, 10 na 5 kwa wanaume na wanawake.


Mshindi wa kwanza wa mbio za kilomita 42 kwa wanaume, Michael Kishiba kutoka JKT Arusha akihitimisha mbio hizo.

Mashindano yaliyofanyika Fort Ikoma yalikuwa maalumu kwa ajili ya kuhamasisha jamii kuacha vitendo vya ujangili, yani Special Ant-poaching.


Mshindi wa pili wa mbio za kilomita 42 kwa wanaume, Moris Mosima kutoka Kenya akihitimisha mbio hizo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi kwa washindi katika viwanja vya Sokoine mjini Mugumu, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Serengeti, Dkt Vicent Mashinji ameahidi kushirikiana na viongozi husika kujenga timu ya riadha ya wilaya hiyo.


Mshindi wa pili wa mbio za kilomita 42 kwa wanawake, Nyamizi Ngassa kutoka Mwanza akihitimisha mbio hizo.

“Tuweke nguvu katika riadhara, tunataka wilaya yetu iwe inatoa ushindani. Niandalieni mpango mniletee tutambue vipaji, tutengeneze timu, tuilee ili tuwe na watu wenye uwezo wa kushindana,” DC Mashinji ameagiza na kuahidi kuchangia shilingi milioni moja mpango huo.

Ameongeza kuwa wilaya hiyo inadhamiria kukuza utalii wa michezo kwa kujenga shule na viwanja vya michezo vyenye hadhi ya kimataifa.



DC huyo ameweka wazi kuwa mipango ya maendeleo atakayoipa kipaumbele ni pamoja na kuhakikisha wilaya hiyo inakuwa kitovu cha mapumziko ya watalii kabla ya kuingia na mara wanapotoka kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Amesema eneo kubwa la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti lipo ndani ya wilaya hiyo, hivyo inapaswa kuongoza kwa upatikanaji wa huduma zinazohitajika kwa watalii, ili kuchochea maendeleo yake.


DC Mashindi (wa tatu kushoto) akikabidhi zawadi kwa mshindi wa kwanza wa mbio za km 42 kwa wanawake, Banueliya Katesigwa kutoka Moshi.


DC Mashindi akiendelea kukabidhi zawadi kwa washindi



Pamoja na mipango ya ujenzi wa uwanja wa ndege na hoteli za kitalii, DC Mashinji amesema viwanja vya michezo vya kisasa ni muhimu kwani vitashawishi wanamichezo wa kimataifa kuchagua wilaya hiyo kama sehemu yao nzuri ya kutembelea kwa ajili ya kupumzika na kufanya mazoezi.


Makabidhiano ya zawadi yakiendelea



Kwa upande wake, Meneja Mradi wa shirika la uhifadhi la Frankfurt Zoological Society (FZS) Serengeti, Masegeri Rurai amesema wao kama wadau wa uhifadhi wameshiriki na kuchangia ufadhili wa mbio hizo.

“Faida ya hizi mbio ni kwamba zinawahamasisha wananchi kushiriki utalii wa ndani katika maeneo ya uhifadhi, lakini zaidi tunawahamasisha kuachana na vitendo vya ujangili na uharibifu wa maliasili katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti,” Rurai amesema.

Amewapongeza wananchi wa Mugumu waliobuni mashindano hayo akisema ni fursa muhimu pia kuwezesha wananchi kupata elimu ya uhifadhi.


Masegeri Rurai (katikati) akikabidhi zawadi kwa mshindi

“Nimeshiriki mbio za kilomita 10 - nimekuwa wa tisa, ninajisikia vizuri kwa sababu kukimbia ni moja ya mazoezi na kunajenga afya, nashauri watu washiriki kwenye mbio hizi.

“Nimekuja na familia yangu yote, niko na mke wangu - amekuwa wa tatu katika mbio za kilomita 10 kwa wanawake na watoto wangu watatu wameshiriki mbio za kilomita tano,” Meneja Mradi huyo wa FZS amesema.



Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya SETCO, Samwel Nyankogoti amesema waliandaa mashindano hayo kupitia taasisi ya michezo ya Serengeti Tourism Sports Agency (SETSA).

“Lengo kuu la mashindano haya ni kuchochea hamasa ya uhifadhi wa ikolojia yetu ya Serengeti na kutangaza utalii wa ndani katika ukanda wetu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

“Malengo yetu mengine ni kutaka watu wafahamu kwamba migration (misafara ya nyumbu) ni kivutio kikubwa katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ambacho hakipatikani sehemu nyingine duniani.

“Kwa hiyo, jamii ione the great migration ni kivutio kikubwa na fursa kubwa ya kiuchumi tuliyo nayo ndani ya wilaya ya Serengeti na mkoa wa Mara,” Nyankogoti amesema.

Washindi wa mbio hizo kwa wanaume na wanawake wamepewa zawadi za medali na fedha taslimu.



Mshindi wa kwanza wa mbio za kilomita 42 kwa wanaume ni Michael Kishiba kutoka JKT Arusha na kwa upande wa wanawake ni Banueliya Katesigwa kutoka Moshi, ambao kila mmoja amezawadiwa medali na Sh 500,000.

Mashindano hayo yamefadhiliwa na wadau mbalimbali, likiwemo shirika la FZS.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages