NEWS

Thursday 9 September 2021

DC Mashinji: Nimepata wawekezaji, wapewe ardhi haraka Serengeti
MKUU wa Wilaya (DC) ya Serengeti mkoani Mara, Dkt Vicent Mashinji (pichani juu), amesema amepata wawekezaji kadhaa wanaoonesha nia ya kuwekeza katika sekta za utalii na elimu ya fundi wilayani hapo.

Akihutubia kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo mjini Mugumu jana, DC Mashinji ameagiza halmashauri hiyo kuharakisha utengaji wa maeneo kwa ajili ya wawekezaji hao, wakiwemo wanaohitaji kujenga hoteli za kitalii katika wilaya hiyo.


DC Mashinji akihutubia kikao hicho

DC huyo amesema anapenda kuona wilaya hiyo inakua kiuchumi na kutumia fursa ya uwepo wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kujitangaza, kuliko mji wa Mugumu ambao ni makao makuu yake. “Serengeti ina brand yake ya kuitangaza, sio Mugumu,” amesema.

Aidha, ameitaka halmashauri hiyo kuharakisha maamuzi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Katika hatua nyingine, Dkt Mashinji amepiga marufuku watoto wanaozurusa mitaani bila kwenda shule na kutahadharisha kuwa hata wazazi wao watachukuliwa hatua za kisheria.


Madiwani kikaoni

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayub Mwita Makuruma amewahimiza madiwani na watendaji kuchapa kazi na kushirikiana katika utumishi wa umma, kwa ustawi wa maendeleo ya halmashauri hiyo.

“Kila mmoja kwa nafasi yake afanye kazi kwa bidii na weledi, ili halmashauri yetu iende vizuri hata katika ukusanyaji mapato na utekelezaji miradi ya maendeleo,” Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ayub Mwita Makuruma amesisitiza.


Mkuruma akizungumza kikaoni

Mkuruma amesema ushirikiano hafifu wa maofisa watendaji na madiwani unachangia miradi ya huduma za kijamii kutekelezwa chini ya kiwango.

“Hatutawavumilia watendaji na madiwani watakaoonesha kutotoa ushirikiano. Halmashauri ni ya madiwani na watendaji,” Makuruma ameongeza.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashgauri (DED) hiyo, Kivuma Hamisi Msangi ameahidi kuimarisha usimamizi kwa watumishi walio chini yake na ushirikiano kwa madiwani.


DED Msangi akizungumza kikaoni

“Ofisi yangu itasimamia vizuri watumishi na kuwapa madiwani ushirikiano wa dhati, ili kuchochea maendeleo ya halmashauri yetu,” DED Msangi amesisitiza.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages