NEWS

Wednesday 6 October 2021

Madiwani Serengeti wataka wataalamu wasiwafiche BOQ za miradi
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti wametoa azimio la kuwataka wataalamu kuwashirikisha kikamilifu, ikiwa ni pamoja na kuwaonesha nyaraka za gharama za miradi (BOQ) ya maendeleo inayotekelezwa katika kata zao.

Wamepitisha azimio hilo wakati wa kikao cha baraza lao mjini Mugumu, kilichoongozwa na Mwenyekiti wao, Ayub Mwita Mkuruma, leo Oktoba 6, 2021.

Awali, kabla ya kupitisha azimio hilo, madiwni hao wamelalamika kwamba wataalamu wamekuwa wakikataa kuwaonesha BOQ, hali ambayo wamesema imekuwa ikitoa mianya ya hujuma na ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo.

“Hili limekuwa ni tatizo kubwa, kwa sababu miradi inatekelezwa na diwani anakuwa hajashirikishwa katika lolote, wakati yeye ndiye mwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya kata,” Makuruma amesema.


Makuruma akizungumza kikaoni

Madiwani hao wamesisitiza suala la kushirikishwa kikamilifu ili iwe rahisi kwao kufuatilia, kusimamia na kuhakikisha kuwa miradi inatekelezwa kwa ufanisi.

Katika azimio hilo, wamemtaka Mkurugenzi Mtendaji kuwaelekeza wataalamu wa halmashauri hiyo kuhakikisha kila diwani anashirikishwa kikamilifu katika kusimamia miradi ya maendeleo.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Wambura Sunday amesema azimio hilo linalenga kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi, hivyo litatekelezwa kama ilivyoelekezwa.

(Habari na zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages