NEWS

Sunday 17 October 2021

Mara yatengewa bilioni 14/- za madarasa, RC Hapi aagiza uundaji kamati za usimamizi


MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Ally Hapi amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo kuunda kamati zitakazosimamia ujenzi wa vyumba vya madarasa zaidi ya 600, uliotengewa Sh bilioni 14 kutoka kwenye mkakati wa kupambana na UVIKO-19 uliozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni.

RC Hapi ametoa agizo hilo jana Jumamosi, wakati akihutubia mikutano ya wananchi kwa nyakati tofauti katika wilaya za Rorya na Tarime, katika ziara yake ya kukagua maandalizi ya ujenzi wa madarasa hayo na vituo sita vya afya mkoani hapa.

“Mkoa wa Mara ni miongoni mwa mikoa mitano iliyopatiwa pesa nyingi kuliko mikoa mingine, tulikuwa na upungufu wa madarasa 618, tutajenga yote likiwemo bweni moja la watoto wenye mahitaji maalumu na vyumba 90 vya shule shirikishi, na kila darasa limetengewa milioni 20,” amefafanua.

Akikagua ujenzi wa kituo cha afya Nyamagaro, Bugendi wilayani Rorya ambacho kitakuwa kinahudumia kata 11, RC Hapi amesema wilaya hiyo imeletewa Sh bilioni 2.3 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 98.

Aidha, akikagua eneo la ujenzi wa vyumba sita vya madarasa katika Shule ya Sekondari ya Nyamtinga wilayani hapo, amewaonya wajumbe wa kamati watakaopeleka mafundi wa ‘mfukoni’, badala ya kutangaza zabuni kwa uwazi, huku akitaka mafundi wa eneo husika wapewe kipaumbele.

“Hizi pesa sio za kumalizia maboma ni za kujenga madarasa mapya, na mafundi watakaohitajika ni wa eneo hilo hilo au wilaya husika ili pesa zibaki mifukoni mwa wananchi, wala hizi pesa sio za kulipa fidia ya eneo, kama shule haina eneo la ujenzi pelekeni shule yenye eneo, hakuna fidia,” amesema.


RC Hapi akielekeza jambo wilayani Rorya

Katika Halmashauri ya Mji wa Tarime iliyokuwa na upungufu wa vyumba 28 vya madarasa, Mkuu huyo wa mkoa amesema imetengewa Sh milioni 560, huku Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) iliyolikuwa na upungufu wa madarasa 116 ikitengewa Sh bilioni 2.3.

Amefananua kuwa mabilioni hayo ni kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, madawati na shule shikizi 120, vinavyotarajiwa kukamilika kabla ya Januari 2022.

(Habari na picha zote: Mobini Sarya wa Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages