NEWS

Sunday 31 October 2021

Mbunge Ghati achangisha mamilioni ujenzi wa Kanisa Katoliki Tarime




MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Ghati Zephania Chomete, leo Jumapili Oktoba 31, 2021 ameshiriki misa takatifu katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi Parokia ya Tarime, kisha kuendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa la Rebu.

Harambee hiyo imefanikisha upatikanaji wa shilingi milioni 30, ambapo Mbunge Ghati na marafiki zake wamechangia shilingi milioni 11.4, zikiwemo fedha taslimu shilingi milioni 8.7 na ahadi shilingi milioni 2.7.

Nao wafanyabiashara maarufu, Christopher Gachuma na Peter Zakaria, kila mmoja amechangia shilingi milioni tano katika harambee hiyo.


Mbunge Ghati (kulia) akimkaribisha mfanyabiashara Zakaria (katikati) na mke wake, Anthonia katika harambee hiyo.

Mbali na michango hiyo, Zakaria amemuunga mkono Mbunge Ghati kwa shilingi milioni moja na mke wake, Anthonia Zakaria amemuunga kwa shilingi laki tano.

Ghati pia amefuatana na madiwani kadhaa wa viti maalum kutoka halmashauri ya Manispaa Musoma ambao wamechangia fedha taslimu.

Mbunge huyo amesindikizwa na marafiki kadhaa kutoka Tarime na Musoma, amesisitiza umuhimu wa kumalizia ujenzi wa Kanisa Katoliki jipya la Rebu, ili kupanua wigo wa mahubiri ya neno la Mungu.


Kwa upande mwingine, mbunge huyo kutoka chama tawala - CCM, amewaomba waumini wa kanisa hilo kuendelea kuunga mkono kaulimbiu ya Rais wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan ya Kazi Iendelee, kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma, Michael Msonganzila naye ameshiriki katika harambee hiyo, ambapo mwenyeji wake amekuwa Paroko wa Parokia ya Tarime, Padre Lucas Chacha.



Mamia ya waumini wa kanisa hilo, wakiwemo wanakwaya (pichani juu) wamechangamsha na kunogesha harambee hiyo kwa shangwe, nderemo na vifijo, huku wakionesha kufurashiwa mno na uwepo wa Mbunge Ghati.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa kanisa jipya la Rebu, Ernest Oyoo amemshukuru Mbunge Ghati kwa kukubali wito wa kuwa mgeni rasmi katika harambee hiyo na kuwataka waumini na wadau mbalimbali kushirikiana kwa hali na mali, ili kufanikisha ujenzi huo.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages