NEWS

Thursday, 6 November 2025

Siku ya Mtoto wa Kike Duniani 2025: AICT, Right to Play wapewa kongole



Wanafunzi wa Shule ya Msingi Nyansincha ya wilayani Tarime wakifurahia zawadi wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani 2025.

Na Joseph Maunya
Akiripoti kutoka
Mara

------------

Wanafunzi wa kike kutoka shule tofauti katika wilaya za Serengeti na Tarime mkoani Mara, wametaja Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Right to Play, kama mkombozi kutokana na jitihada zao za kuelimisha jamii faida za kusomesha watoto wa kike.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Nyansincha - Tarime na Shule ya Msingi Merenga B – Serengeti, walizipongeza AICT na Right to Play wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani mwaka huu, yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule hizo kwa nyakati tofauti chini ya ufadhili wa taasisi hizo.


Wanafunzi wakionesha umahiri wa kucheza ngoma ya asili wakati wa maadhimisho

"Hawa wageni wetu (AICT, Right to Play) wamekuwa ni kama wakombozi kwetu sisi watoto wa kike, maana kwa sasa wazazi hawatulazimishi tena kuolewa, badala yake wanatusisitiza kusoma," alisema Rosemary Nyamohanga, mwanafunzi wa darasa la sita Shule ya Msingi Nyansincha.

"Nawashauri wazazi wengine ambao bado wanaamini kwamba mtoto wa kike anafaa tu kuolewa waache ili wawasaidie watoto wao wafikie ndoto zao na kuwa msaada kwa familia zao na taifa pia," alisema Sarah Mgeta, mwanafunzi wa darasa la tano Shule ya Msingi Merenga B.

Afisa Mradi kutoka AICT, Daniel Fungo, alisema lengo lao ni kuwasaidia watoto wa kike kuondokana na ukandamizwaji wa haki zao, hasa haki ya kupata elimu kama ilivyo kwa watoto wa kiume.


Afisa Mradi kutoka AICT, Daniel Fungo, akizungumza katika maadhimisho hayo.


"Sisi (AICT) tunashirikiana na Right to Play ili kuhakikisha watoto wa kike pia wanapewa haki zao za msingi, ikiwa ni pamoja na haki ya kupata elimu kama watoto wa kiume, maana wote ni sawa na hawapaswi kubaguliwa," alisema Fungo.

Alifafanua kuwa taasisi hizo zinatoa elimu ya uhamasishaji kwa jamii kupitia matamasha ya michezo shuleni, ambapo mbali na elimu, pia wanatoa zawadi za vifaa vya michezo na vinywaji baridi kwa wanafunzi.


Wanafunzi wa Shule ya Msingi Merenga B wakipokea zawadi. (Picha zote na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages