NEWS

Monday 25 October 2021

Mradi wa umeme Rusumo: Wadau waafikiana kutatua changamoto zilizopo




WADAU wa mradi wa maporomoko ya umeme Rusumo upande wa Tanzania (pichani juu), wamekutana wilayani Biharamulo, Kagera kuangazia maendeleo ya mradi huo, changamoto zilizopo na ufumbuzi wake.

Wadau hao ni viongozi wa kijamii na taasisi za umma, TNDF, NELSAP na wananchi wanaozunguka mradi huo kutoka maeneo ya Rusumo na wilaya ya Ngara mkoani Kagera.



Wamekutana mjini Biharamulo Ijumaa iliyopita na kukubaliana kushirikiana katika kutatua changamoto zilizopo kwa wakati.

Changamoto kubwa zilizotajwa na zinazohitaji ufumbuzi wa haraka ni malipo ya fidia za nyumba na mashamba ya wananchi, vilivyoathiriwa na shughuli za utekelezaji wa mradi huo.



Ofisa Maendeleo ya Jamii na Makazi kutoka NELSAP, Gaspar Mashengiya amekiri kuwepo kwa uharibifu wa baadhi ya nyumba za makazi ya watu wakati wa milipuko ya kuvunja miamba ili kujenga nyumba ya umeme na handaki la kupitisha maji.

Mashengiya amesema changamoto nyingine ilitokana na mafuriko yaliyoharibu baadhi ya mashamba ya mazao mbalimbali mwaka 2018 na ukwepeshaji mto ili kujenga handaki.


Mashengiya (aliyesimama) akizungumza kikaoni

“Kwa upande wa milipuko, tumeunda kamati inayoendelea kushughulikia, lakini tayari mradi umeshakarabati na kujenga nyumba 22.

“Kwa sasa mradi unaendelea kutambua nyumba nyingine zilizoonekana kuwa na changamoto zaidi ili ziingizwe kwenye awamu ya pili ya mpango wa ukarabati na ujenzi.

“Kuhusu mafuriko, tayari mradi umeshafanya uthamini kwa mashamba zaidi ya 1,160, umepokea malalamiko mengine 91 na tayari yameshafanyiwa uchunguzi na hivi karibuni wananchi husika watapewa mrejesho ili wanaostahili wafanyiwe uthamini," Mashengiya amesema.



“Ni shauku yetu kuhakikisha kwamba fidia zinalipwa kwa wakati na tunategemea kabla ya mwisho wa mwaka 2021, fidia iwe imeshalipwa kwa waliopata madhara ya mafuriko,” Mashengiya amesema.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Rusumo unapotekelezwa mradi wa umeme Rusumo, Pascary Opodi ameomba michakato ya ulipaji fidia iharakishwe ili kuondoa malalamiko na manung’uniko kwa wananchi walioathiriwa.


Opodi (aliyesimama) akizungumza kikaoni

Hata hivyo, Mtaalamu wa masuala ya jamii na mazingira katika mradi wa umeme Rusumo, Nassor Mulika amesema wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka mradi huo wametekelezewa miradi ya afya, elimu, maji, ufugaji, chuo cha maendeleo ya wananchi, uwanja wa michezo, kilimo na ushonaji nguo.


Mulika akisisitiza jambo kikaoni

Mradi wa maporomoko ya umeme Rusumo ni mali ya nchi za Tanzania, Burundi na Rwanda, unaotekelezwa na NELSAP chini ya Nile Basin Initiative (NBI) ambao ni muungano wa nchi 10 zilizopo katika Bonde la Mto Nile.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Jumuiko la Asasi Zisizo za Kiserikali katika Bonde la Mto Nile Upande wa Tanzania (Tanzania Nile Discourse Forum – TNDF) na Katibu Mkuu wa Kusanyiko la Asasi za Kiraia katika Bonde la Mto Nile (Nile Basin Discourse – NBD), Dkt Donald Kasongi, mradi huo unafadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) kwa gharama ya Dola za Kimarekani milioni 340.



“Mradi huu ukikamilika utakuwa na uwezo wa kutoa megawati 80 za umeme zitakazogawanywa kwa nchi za Burundi, Rwanda na Tanzania, kila moja ikipata megawati 27.

“Hadi sasa ujenzi wa mradi huu wa umeme Rusumo umeshakamilika kwa asilimia 81,” Dkt Kasongi amefafanua.


Dkt Kasongi akizungumza kikaoni

Kwa upande wake, Helena Adrian kutoka shirika lisilokuwa la kiserikali la Lake, ameshauri wadau kuimarisha ulinzi na utunzaji wa vyanzo vya maji katika maeneo husika, ili kuwezesha mradi huo kuwa endelevu, kwa manufaa wa nchi zote tatu.

“Mazingira yatunzwe kwa kupanda miti na wananchi wahamasishwe kuepuka uharibifu wa vyanzo vya maji,” amesema.



(Habari na picha zote: Christopher Gamaina, Biharamulo)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages