
Dhahabu
Na Mwandishi Wetu
Tanzania imeibuka na kushika nafasi ya tatu kati ya nchi tano za Afrika zinazolisha dhahabu kwa wingi, kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni kwa mwaka unaoishia Agosti 2025, zilizotolewa na gazeti la Vanguard News la Nigeria wiki iliyopita.
Dhahabu inabakia moja ya bidhaa muhimu za Afrika zinazouzwa nchi za nje kwa mwaka 2025, nchi ambazo zimekuwa zikizalisha dhahabu na nyingine zinazochomoza na kutawala uuzaji wa madini hayo.
Tanzania imejipatia umaarufu wa kuwa muuzaji wa dhahabu barani Afrika, huku takwimu zikionesha kuwa kwa mwaka ulioishia Agosti 2025 iliuza dhahabu yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 4.32, ikilinganishwa na dola bilioni 3. 19 kwa mwaka 2024.
Ongezeko hilo limechochewa na kuongezeka kwa bei ya dhahabu duniani pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji na ushiriki wa kampuni kubwa na wachimbaji wadogo.
Dhahabu ni moja ya bidhaa za Tanzania zenye thamani kubwa zinazouzwa nje ya nchi na kuingiza fedha nyingi za kigeni.
Nchi nyingine za Afrika zinazozalisha na kuuza dhahabu nje kwa mpangilio wa uzalishaji ni Ghana, Afrika Kusini, Burkina Faso na Mali.
Kwa mwaka 2025, mauzo ya dhahabu yanaendelea kuchochea ukuaji wa uchumi kwa nchi za Afrika, licha ya kuwepo changamoto mbalimbali ambazo hata hivyo haziathiri ukuaji wa uchumi.
No comments:
Post a Comment