NEWS

Monday 18 October 2021

Msajili wa Jumuiya kupiga kambi Mwanza kuhuisha usajili wa zisizo za kidini Kanda ya Ziwa
VIONGOZI na wanachama wa jumuiya zisizo za kidini kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, wanaombwa kujitokeza kuhuisha vyeti vya jumuiya zao zilizosajiliwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma, iliyotolewa Oktoba 16, 2021 na Msajili wa Jumuiya kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Emmanuel Kihampa (pichani juu), uhuishaji huo utafanyika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kuanzia Oktoba 20 hadi 28, 2021.

Kihampa amefafanua kuwa jumuiya zinazolengwa katika shughuli hiyo ni pamoja na za kiutamadani, kijamii, kiuchumi, kitaaluma, vyama na vikundi vinavyoeneza mila na desturi mbalimbali, vikiwemo vya kufa na kuzikana, kusaidiana, ujirani mwema, ujasiriamali, kilimo, ufugaji na stadi za kazi.

Amesisitiza kuwa viongozi na wanachama wa jumuiya hizo kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, ambayo ni Mwanza, Mara, Kagera, Shinyanga, Geita na Simiyu, wanapaswa kujitokeza kushiriki kikamilifu katika uhuishaji wa vyeti vyao vya usajili.

Msajili huyo ameendelea kufafanua kuwa shughuli hiyo itahusisha uwasilishaji wa vyeti halisi vya usajili na nakala zake, taarifa za mapato na matumizi, taarifa za utendaji kipindi cha miaka mitano iliyopita, uthibitisho wa malipo ya ada kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, taarifa ya mwisho ya mabadiliko ya uongozi, katiba na kanuni za jumuiya husika.

“Lakini pia, viongozi na wanachama watakaoshiriki katika zoezi hili watapaswa kufanya malipo ya shilingi 100, 000 ili waweze kupatiwa cheti kipya,” ameongeza.

Kihampa amesisitizo kwamba viongozi na wanachama wa jumuiya zote zisizo za kidini zilizosajiliwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, zilizopo Kanda ya Ziwa zinapaswa kushiriki kikamilifu katika shughuli hiyo, huku akitahadharisha kuwa kutokushiriki kwao kunaweza kusababisha usajili wa jumuiya husika kufutiwa usajili wake na kuondolewa kwenye Rejista ya Usajili, kwa mujibu wa Sheria ya Usajili wa Jumuia - Sura Na. 337.

“Ikumbukwe kwamba zoezi hili [la uhuishaji wa vyeti vya usajili] halibadilishi historia wala kumbukumbu ya jumuiya husika, bali kinachobadilishwa ni hadhi ya vyeti vya usajili kutoka kuwa vya kudumu na sasa vitakuwa vinahuishwa kila baada ya miaka mitano,” Kihampa amebainisha katika taarifa hiyo.

Pia Kihampa ametoa wito kwa viongozi jumuia na vikundi vyote vyenye sifa ya kusajiliwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika Ofisi ya Msajili, kufika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kati ya Oktoba 20 na 28, 2021 ili kupatiwa utaratibu wa kuvisajili, lakini pia kuweza kusajili vyama na vikundi ambavyo tayari vimekamilisha taratibu za kusajiliwa.

Msajili huyo amewataka viongozi na wanachama wa jumuiya hizo wenye maoni na wanaohitaji ufafanuzi zaidi, kuwasiliana na ofisi yake kwa piga namba ya simu 0734712744, au kutuma ujumbe kupitia barua pepe: rs@moha.go.tz

#MaraOnlineNews-Updates

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages