NEWS

Monday 18 October 2021

Wanavijiji ruksa kutumia buffer zone, Serikali yawataka kuheshimu mipaka ya Hifadhi ya Taifa SerengetiWaziri William Lukuvi

SERIKALI imeruhusu wakazi wa vijiji vilivyo jirani na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti katika wilaya za Serengeti na Tarime mkoani Mara, kutumia eneo kinga (buffer zone) kwa shughuli za maendeleo, ikiwemo kulisha mifugo.

Uamuzi huo wa Serikali umetangazwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi wakati wa ziara yake mkoani hapa, wiki iliyopita.

Hata hivyo, Waziri Lukuvi amesema hatua hiyo haijavunja Tangazo la Serikali (Government Notes - GN) la mwaka 1968, linalotambua na kutaka mipaka ya hifadhi hiyo izingatiwe na kuheshimiwe.

Tamko hilo la Serikali linavihusu vijiji vya Bisarara, Bonchugu, Nyamakendo, Nyamburi, Machochwe, Mbalibali na Merenga (Serengeti), Masanga, Gibaso, Kegonga, Kenyamosabi, Nyandage, Nyabirongo na Karakatonga (Tarime).


Muonekano wa milima katika kimojawapo cha vijiji vya wilayani Tarime, vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti upande wa Kaskazini, ambapo kwa sasa ni msimu wa kuonekana kwa makundi makubwa ya nyumbu.

Waziri Lukuvi ameagiza viongozi na wataalamu husika, wakiwemo kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kushirikiana na wakazi wa vijiji hivyo kuelekezana namna nzuri ya kutumia buffer zone bila kuingilia mipaka ya hifadhi hiyo.

Waziri Lukuvi amebainisha kuwa uamuzi wa kuruhusu wanavijiji kuendelea kutumia buffer zone ni matokeo ya kazi iliyofanywa na kamati maalum ya mawaziri wanane iliyoundwa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt John Pombe Magufuli ili kupitia na kutafuta ufumbuzi wa migogoro ya ardhi, inayotokana na mwingiliano wa vijiji na hifadhi za taifa, mashamba ya Serikali, ranchi na vyanzo vya maji.

Baadaye Mara Online News imewasiliana na Waziri Lukuvi kwa njia ya simu ili kupata ufafanuzi zaidi, ambapo amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imeamua wananchi wasiondolewe ndani ya buffer zone na siyo kuingilia mipaka wala kumegewa eneo la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Wanyamapori wakifurahia mandari ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti

“Hakuna hifadhi inayomegwa. Mipaka na maeneo ya hifadhi yataendelea kulindwa kwa mujibu wa sheria na GN (Tangazo la Serikali) ya mwaka 1968.

“Kwa hiyo, wanavijiji waelewe vizuri jambo hili wasije wakaingia kwenye hifadhi,” Waziri Lukuvi amesisitiza katika mazungumzo hayo.

Naye Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Masana Mwishawa hakwenda nje ya msimamo wa Serikali alipozungumza na Mara Online News kwa njia ya simu pia.

“Hifadhi na maeneo yake yote yataendelea kusimamiwa kama ilivyo kwenye GN ya mwaka ‘68. Kitachokabidhiwa kwa wananchi ni eneo la kinga, yaani buffer zone, ambalo ni eneo lililo nje ya hifadhi,” Mhifadhi Mwishawa amesema.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara, Oktoba 18, 2021

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages