NEWS

Monday 18 October 2021

Musoma Vijijini wanavyojizatiti kuboresha kilimo, Mbunge Muhongo awapiga jeki plau kupunguza jembe la mikono




WANANCHI wa jimbo la Musoma Vijijini katika mkoa wa Mara, wanaendelea na juhudi za kuboresha kilimo kwa njia mbalimbali, ikiwemo kutumia plau (jembe la kukokotwa na ng’ombe).

Walianza kwa kuunda vikundi vya kilimo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kilimo, kama vile pembejeo, mikopo na ushauri.

Kisha wakaweka mkazo kwenye kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia maji ya Ziwa Victoria na mito isiyokauka.

Baadaye wakaongeza matumizi ya plau na kupunguza matumizi ya jembe la mkono.

Fedson Masawa, Verediana Mgoma, Hamisa Gamba na Vaileth Peter ni wasaidizi wa Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo.

Wanasema hadi sasa vikundi 362 vya kilimo vimeshaundwa katika kata zote 21 zinazounda jimbo hilo.

Wanataja kata hizo na vikundi vyake vikiwa kwenye mabano kuwa ni Bugoji (13), Bugwema (14), Bukima (32), Bukumi (47), Bulinga (7), Busambara (9), Bwasi (9), Etaro (21) na Ifulifu (9).

Kata nyingine ni Kiriba (24), Makojo (27), Mugango (28), Murangi (7), Musanja (7), Nyakatende (12), Nyambono (6), Nyamrandirira (14), Nyegina (37), Rusoli (5), Suguti (24) na Tegeruka (10).



Wakizungumzia kilimo cha umwagiliaji, wanasema vijiji vingi vya jimbo la Musoma Vijijini viko karibu na Ziwa Victoria.

“Kwa hiyo, kwa sasa, kilimo cha umwagiliaji kinawekewa mkazo sana, na wakulima wamekubali kufanya kilimo hiki,” Fedson Masawa anasema.

Anaongeza “Baadhi ya vikundi vya kilimo vilivyoko pembezoni mwa Ziwa Victoria vimejinunulia vyenyewe vifaa vya umwagiliaji, zikiwemo pampu na mipira ya kumwagilia.”


Kwa mujibu wa wasaidizi hao wa mbunge, vikundi 15 vilipewa pampu, mipira na mbegu kutokakana na fedha za Mfuko wa Jimbo.

Vikundi hivyo, wanasema ni kutoka kata za Bugwema, Bukima, Bukumi, Busambara, Bwasi, Etaro, Kiriba Makojo, Mugango, Murangi, Musanja, Nyakatende, Nyegina, Nyambono na Suguti.



Jembe la kukokotwa na ng'ombe (plau)
Hii ni programu iliyoanzishwa na Mbunge Muhongo ili kupunguza matumizi ya jembe la mkono katika kilimo jimboni.

Hadi sasa Mbunge huyo ameshagawa bure plau 85 kwenye vikundi 85 vya kilimo kutoka kata zote 21.

“Programu hii ni endelevu,” Profesa Muhongo anasema.



Jitihada hizo zimezaa mafanikio na matokeo chanya kwa wakulima walio kwenye vikundi.

Wanachama wa vikundi vya kilimo wanataja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kupanua mashamba yao, kutoka ekari moja hadi tano, au zaidi kwa kila mkulima mdogo.

Wakulima wanaoendelea kutumia jembe la mkono ni wale wenye mashamba madogo madogo.

“Jitihada hizi zimesaidia pia kuokoa muda wa kazi shambani - kwa kutumia kipindi kifupi kulima kwa kutumia plau badala ya jembe la mkono,” Varediana Mgoma anasema.

Baadhi ya vikundi vya kilimo vimeweza kugawa sehemu ya mavuno yao ya mazao ya chakula kwenye shule za maeneo yao.

Kuongezeka kwa mavuno ya kilimo na mapato ya fedha kwa wanachama wa vikundi vya kilimo, kumewawezesha kusomesha watoto wao ipasavyo, kufungua biashara mpya, kukopeshana fedha na kujenga nyumba bora.

Kwa sasa, wakulima katika jimbo la Musoma Vijijini wanataka kupiga hatua ya kuelekea kwenye kilimo cha kutumia matrekta.

“Kwenye kipindi hiki cha mpito, wanaomba wadau wa maendeleo, ikiwemo Halmashauri Wilaya ya Musoma kuungana na Mbunge Muhongo kuwagawia plau ili waweze kupunguza matumizi ya jembe la mkono.

Jimbo la Musoma Vijijini linaundwa na kata 21, zenye vijiji 68.

Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo

(Na Mwandishi wa Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages