NEWS

Saturday 20 November 2021

Ajira jumuishi: TAYOHADO yataka watu wenye ulemavu wasitengwe




SHIRIKA la Afya na Maendeleo ya Vijana Tanzania (TAYOHADO) limetoa wito kwa Serikali na taasisi za kiraia kuboresha mifumo ya ajira na miundombinu isiyo na ubaguzi kwa watu wenye ulemavu.

TAYOHADO imetoa wito huo katika mkutano na wanahabari mjini Tarime leo Novemba 20, 2021, wakati ikitoa mreshesho wa utafiti ilioufanya kupitia mradi wa ajira jumuishi kwa watu wenye ulemavu.

“Serikali itoe elimu inayohusisha kutengeneza sera na miongozo, vipeperushi na mabango kwa ajili ya kuelimisha jamii kwamba watu wenye ulemevu wanaweza kufanya kazi kama watu wengine.

“Tunasisitiza hili kwa sababu watu wenye ulemavu wanapokwenda kuomba kazi kwenye taasisi mbalimbali hawapati mapokezi mazuri, yaani wanaonekana kama ni watu ambao hawawezi kufanya kazi yoyote ile.

“Tunapaswa kuwajumuisha watu wenye ulemavu katika shughuli zetu, kwa sababu wana talanta ambayo wamepewa, wana vitu vya ziada ambavyo wamepewa na Mwenyezi Mungu.

“Jamii ielimishwe kuwatambua watu wenye ulemavu kwamba wana uelewa kama watu wengine na ni watu ambao wana juhudi kubwa katika kufanya kazi,” Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini wa TAYOHADO, Machera Mkono amesisitiza.


Mkono (kushoto) akizungumza mkutanoni

Kwa mujibu wa Mkono, utafiti walioufanya katika vijiji vya Nyamongo, Nyamwaga, Itiryo na Sirari wilayani Tarime, ubebaini kuwa watu wengi hawaamini kwamba watu wenye ulemavu wanaweza kufanya kazi kama watu wengine katika jamii.

Aidha, amesema miundombinu iliyo rafiki kwa watu wenye ulemavu pia ni changamoto kubwa katika ofisi nyingi za Serikali na taasisi za kiraia. “Ofisi nyingi zina ngazi ndefu zisizo rafiki kwa watu wenye walemavu,” amesema.

Pia, amesema utafiti umebaini kuwa baadhi ya watu wamejenga dhana kwamba mlemavu akionekana kwenye ofisi fulani anakuwa amekwenda kuomba msaada, kumbe wakati mwingine amekwenda kufuatilia haki zake mbalimbali.

“Tumegundua pia kwamba hata kwenye suala la mikopo, watu wenye ulemavu hawajaangaliwa sana, ingawa nao wanastahili kupewa mikopo kupitia asilimia mbili kati ya 10 inayotolewa kwenye halmashauri kutokana na mapato ya ndani,” ameongeza.

Kwa mujibu wa Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini huyo wa TAYOHADO, idadi kubwa ya watu wenye ulemavu katika maeneo ya vijiji hawajui kwamba kuna mikopo inayotolewa na halmashauri kwa ajili yao.

“Wengi wao hawajajua hilo, ingawa ile mikopo ni changamoto, ina masharti mengi na bajeti yake ni finyu, ilitakiwa kuwa angalau asilimia tano na wapunguziwe masharti,” Mkono amesema.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi huo, Marwa Mwita amesema wanaendelea kutoa elimu ya kuhamasisha makundi ya rika, jinsi na hali zote kuwathamini watu wenye ulemavu na kuwashirikisha katika shughuli mbalimbali.


Mwita (kulia) akizungumza kutanoni

Mwita amefafanua kuwa wanatumia mikutano mbalimbali kama vile semina na makangamano kueneza elimu hiyo kupitia mradi wa ajira jumuishi kwa watu wenye ulemavu, chini ya ufadhili wa Shirika la INTERNEWS.

“Kwa maeneo ya vijijini ambako tumezunguka, tumekuta tatizo ni kubwa, watu wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto nyingi. tunaomba wadau wengine wajitokeze kuunga mkono Shirika la INTERNEWS kutufadhili katika shughuli hizi,” Mwita amesema.

(Habari na picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages