NEWS

Monday 8 November 2021

Kasi ujenzi mradi wa maji Mugango - Kiabakari: Naibu Katibu Mkuu Eng Kemikimba akagua maendeleo yake




NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba amekagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wa Mugango - Kiabakari utakaosambaza huduma ya maji safi ya bomba kutoka Ziwa Victoria kwa maelfu ya wananchi katika halmashauri za wilaya za Musoma Vijijini na Butiama mkoani Mara.



Mhandisi Kemikimba ambaye ameongozana na Mkurugenzi wa Idara ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Wizara ya Maji, CPA Joyce Msiru, ametumia saa kadhaa mapena leo Novemba 8, 2021 kukagua maeneo mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa tenki ambao umefikia asilimia 85.


Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya Maji Mugango - Kiabakari, Eng Cosmas Sanda (wa pili kutoka kulia) akitoa maelezo kuhusu mradi huo kwa Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Kemikimba (kushoto). Katikati ni CPA Msiru.

Utekelezaji wa mradi huo utagharimu shilingi bilioni 70.5, huku ujenzi wake ukitarajiwa kukamilika mwakani (2022).


Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Kemikimba (katikati) akipokea maelezo juu ya mradi huo kutoka kwa mkandarasi. Kulia ni CPA Msiru.

Wananchi 164,900 wanatarajiwa kunufaika na mradi huo, hivyo kuwaondolea wananchi wa Butiama na Musoma Vijijini kero ya maji.

Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo na wananchi wa jimbo hilo wamekuwa wakiishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutenga mamilioni ya fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kuwasambazia huduma ya maji safi ya bomba kutoka Ziwa Victoria.

Miongoni mwa miradi hiyo, ni ule wa vijiji vya Bugoji, Kaburabura na Kanderema, unaotekelezwa kutokana na fedha za kupambana na KOVID-19 - kiasi cha shilingi milioni 500.

(Na Mwandishi wa Mara Online News, Musoma)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages