NEWS

Saturday 6 November 2021

Ngicho azindua shule ya Rungu Light, aichangia milioni 3/-




MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime mkoani Mara, Daudi Ngicho amezindua rasmi Shule ya Msingi Rungu Light iliyopo kijijini Gibaso, kilomita chache kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Uzinduzi huo ulifanyika Ijumaa iliyopita, sambamba na mahafali ya wahitimu wa darasa la saba na la awali, ambapo Ngicho ameipiga jeki shule hiyo kwa Sh milioni 3.127, zikiwemo Sh milioni tatu alizotoa yeye binafsi na Sh 127,000 alizoungwa mkono na wageni kadhaa, akiwemo Diwani wa Kata ya Kwihancha, Ragita Ragita.

Ngicho (kulia) akikabidhi fedha hizo kwa Mkurugenzi wa Shule hiyo, Samwel Rungu. Katikati ni Katibu wa UVCCM Wilaya ya Tarime, Newton Mwongi ambaye amefuatana na Mwenyekiti huyo katika sherehe hizo.

Uzinduzi huo pia umefanyika sambamba na kusherehekea matokeo mazuri ya darasa la saba katika mtihani wa taifa mwaka huu (2021), ambapo Shule ya Msingi Rungu Light imeongoza katika kata ya Kwihancha, imekuwa ya 6 kiwilaya na ya 17 kimkoa.


Wahitimu wa darasa la awali shuleni hilo

Ngicho ameeleza kufurahishwa uwepo wa shule hiyo kwa ajili ya kuisaidia jamii ya Gibaso akisema “Ukikosa elimu uwezekano wa kukosa fursa ni mkubwa. Wewe mtoto unayenisikia kazi yako ni kusoma na wewe mzazi unayenisikia kazi yako ni kumsomesha mtoto ili baadaye akusaidie, mfanye mtoto apende shule.”

Ameongeza “Kila jambo lina wakati wake, na mtu hatakiwi kuchanganya mambo, wakati wa kutafuta elimu sio wakati wa kutafuta pesa, ukitafuta pesa wakati wa kutafuta elimu na ukakosa, utakuta muda wa kutafuta elimu umekupita na utajutia.”


Mwenyekiti Ngicho (kulia) na Mkurugenzi Rungu (katikati)

Naye Mkurugenzi wa Shule ya Msingi Rungu Light, Samwel Rungu amewashukuru wadau wote waliojitokeza kuhudhuria na kumuunga mkono katika sherehe hizo.

“Ninawashukuru kwa kuja kuungana nasi katika siku hii muhimu, ninatoa wito kwa wazazi wote kuleta watoto katika shule yetu, kwani tutawapa elimu iliyo bora,” Rungu amesema.

(Na Asteria John wa Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages