NEWS

Friday 5 November 2021

Viongozi Serengeti wafafanua Sh bilioni 2/- za madarasa




VIONGOZI wa umma wilayani Serengeti wamesema Sh bilioni 2.04 zilizotolewa na Serikali kwa idhini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, hazizuii wananchi kuchangia nguvu kazi pale itakapohitajika.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayub Mwita Makuruma na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Kivuma Hamisi Msangi wametoa ufafanuzi huo katika kikao cha baraza la madiwani mjini Mugumu, leo Novemba 5, 2021.



Makuruma na Msangi wametoa ufafanuzi huo kujibu swali la Diwani wa Kata ya Manchira, Michael Kinani aliyewasilisha hoja kwamba baadhi ya wananchi wanakataa kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa, kwa maelezo kuwa Rais Samia ameshatoa fedha, lakini pia Waziri wa TAMISEMI alishakataza wananchi kuchangishwa kwenye miradi ya maendeleo.

Msangi ndiye ameanza kujibu hoja hiyo kwa kusema “Waziri hajakataza wananchi kuchangia maendeleo, alichokataza ni kutoa adhabu kwa walioshindwa kuchangia.”


Msangi akizungumza kikaoni

Naye Makuruma amesema kwamba pale ambapo itaonekana fedha zilizotolewa na Rais Samia zinatosha kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa, wananchi hawana sababu ya kuchangia chochote.

“Lakini mkiona hizo fedha hazitoshi kukamilisha ujenzi kwa ubora unaotakiwa, ni muhimu wananchi kuchangia nguvu kazi bila kulazimishwa,” Makuruma amesisitiza.


Makuruma akisisitiza jambo kikaoni

Awali, kabla ya hoja hiyo kuibuka, Makuruma amekiambia kikao hicho cha madiwani kwamba Serikali chini ya Rais Samia imeipatia halmashauri hiyo Sh bilioni 2.04 kwa ajili ya kugharimia ujenzi wa vyumba vya madarasa 202 katika shule za sekondari.

Kwa upande wa shule za msingi, Katibu Tawala wa Wilaya ya Serengeti, Cosmas Qamara amesema Serikali imetoa Sh milioni 340 kugharimia ujenzi wa vyumba 17 vya madarasa.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages