NEWS

Wednesday, 17 December 2025

Dkt. Nyansaho akabidhi ofisi kwa Mwenyekiti mpya Bodi ya Wakurugenzi TANESCO



Dkt. Rhimo Nyansaho (kulia) akikabidhi ofisi kwa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO, Plasduce Mbossa.

Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
-------------------

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Taifa la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt. Rhimo Nyansaho ambaye kwa sasa ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), amekabidhi rasmi ofisi kwa Mwenyekiti mpya wa Bodi hiyo, Plasduce Mbossa.

Hafla ya makabidhiano hayo ya ofisi ilifanyika Jumanne, Desemba 16, 2025 jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya TANESCO.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Nyansaho aliwashukuru wajumbe wa Bodi na Menejimenti ya TANESCO kwa ushirikiano waliouonesha katika kipindi chote cha uongozi wake, ambapo pia alimhakikishia Mwenyekiti mpya Mbossa kwamba Bodi hiyo iko imara na anaamani ataendeleza pale alipoishia.

“Kwa dhati naishukuru sana Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya TANESCO kwa ushirikiano mlionipatia katika kipindi chote tulichokuwa pamoja. Tulishirikiana kwa karibu kutatua changamoto na kuhakikisha Shirika linasonga mbele katika kuwahudumia wananchi,” alisema Waziri Nyansaho.


Picha ya pamoja

Kwa upande wake Mbossa alimpongeza Dkt. Nyansaho akisema ameiacha TANESCO katika mwelekeo na usimamizi mzuri baada ya miradi mingi mikubwa ya umeme kukamilika, ikiwemo ule wa kimkakati wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uzalishaji na upatikanaji wa umeme nchini.

Vilevile, Mbossa alipongeza jitihada zinazofanywa na TANESCO katika kuboresha huduma kwa wateja, ambazo zimeongeza ufanisi na kumfanya mteja kuwa kipaumbele.

“TANESCO ipo katika mweleko mzuri, miradi mingi ya umeme imekamilika na kuwezesha nchi kuwa na umeme wa kutosha. Tutaendelea kufanya jitihada za kuongeza uzalishaji wa umeme ili kuendana na kasi ya ongezeko la mahitaji ya umeme nchini,” alisema.

Naye Naibu Mkurugenzi Mtendaji (Uzalishaji), Mhandisi Antony Mbushi, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, alimshukuru Dkt. Nyansaho kwa uongozi na ushirikiano wake mzuri, na kusema Menejimenti itaendelea kusikiliza na kutekeleza maelekezo ya Mwenyekiti wa Bodi wa sasa kwa maslahi ya Shirika na Taifa kwa ujumla.

Wakati wa uongozi wake, Dkt. Nyansaho alisimamia utekelezaji wa miradi mingi ya umeme na kuhakikisha imekamilika, ikiwemo Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere, Rusumo, Mradi wa Kusafirisha Umeme wa Lemuguru, miradi mbalimbali ya Gridi imara, kuingiza mikoa ya Kigoma na Katavi kwenye Gridi ya Taifa.

Pia, Dkt. Nyansaho huku ameacha miradi mingine mingi ikiwa katika hatua nzuri za utekelezaji, ukiwemo ule wa Umeme wa Jua wa Kishapu - ambao kwa sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 84.

Katika kipindi cha Dkt. Nyansaho kama Mwenyekiti wa Bodi, TANESCO imefanikiwa kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi wake - jambo limechangia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Shirika na maboresho makubwa ya eneo la huduma kwa wateja, ikiwemo maboresho ya kituo cha miito ya simu, uwepo wa namba 180 ya huduma kwa wateja na mfumo wa Jisoti kuimarisha mawasiliano.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages