NEWS

Monday 1 November 2021

Wadau washiriki mbio za Serengeti Run for Girls kuwezesha wasichana, wanawake Serengeti na Bunda



MBIO za ‘Serengeti Run for Girls’ 2021 zimefanikisha upatikanaji fedha za ufadhili wa masomo kwa wasichana 80 kutoka vijiji vilivyo jirani na mapori ya akiba ya Ikorongo/Grumeti katika wilaya za Serengeti na Bunda.

Mbio hizo ambazo ni mwendelezo wa mpango wa Shirika la Grumeti Fund, zimefanyika kwa siku tatu mfulilizo wiki iliyopita, zikihusisha wanawake wanane raia wa Marekani, wakiwemo Rhonda Vetere, Maya na mmoja kutoka Afrika Kusini.



Wanawake hao wamekimbia umbali wa kilometa 21 kila siku na kuelezea kufurahishwa kwa na mbio hizo ambazo huandaliwa na Shirika la Grumeti Fund kila mwaka.

“Hii ni habari nzuri ya kusimulia, na hakika nitashiriki tena mwaka ujao,” Maya amesema.

Pia wanawake wengine wawili Watanzania, Esther Magambo na Ellena Saronge ambaye ni mfanyakazi wa mapori ya akiba ya Ikorongo/Grumeti wameshiriki mbio hizo.

“Kuna tofauti ya kukimbia porini na kukimbia mjini. Porini unavuta hewa ambayo ni natural (ya asili) na katika mazingira mazuri,” Ellena amesema mara baada ya kushiriki mbio hizo.


Rhonda Vetere (kulia) na Ellena Saronge

Esther Magambo (katikati)

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Shirika la Grumeti Fund, Bhoke Mtatiro amesema lengo la mbio hizo ni kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwezesha wasichana na wanawake katika masomo na ujasiriamani.



“Kwa mwaka huu hizi fedha zitasaidia kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa kike 80 na kugharimia mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake,” Bhoke amesema.



Bhoke ameishukuru Serikali kwa ushirikiano inaolipatia Shirika la Grumeti Fund kupitia taasisi zake, ikiwemo Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA).



Grumeti Fund ni shirika lisilo la kiserikali lililojikita katika kusaidia maendeleo ya jamii na uhifadhi wa wanyamapori kwenye mapori ya akiba ya Ikorongo/Grumeti, Magharibi mwa Serengeti.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

1 comment:

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages