NEWS

Monday 6 December 2021

TNDF, wadau wajadili mustakabili wa uhifadhi Bonde la Mto MaraWADAU wa Bonde la Mto Mara kutoka wilaya tano za Tanzania zinazopitiwa na Bonde hilo, wamekutana kujadili majanga ya kimazingira yanayotishia uhai wa bonde hilo na kupendekeza mbinu za kulinusuru.

Warsha hiyo imeandaliwa na kuendeshwa na Jumuiko la Asasi Zisizo za Kiserikali katika Bonde la Mto Nile (NDF), kupitia Jumuiko la Asasi Zisizo za Kiserikali katika Bonde la Mto Nile Nchini Tanzania (TNDF).“Warsha hii ni muhimu kwa mustakabili wa uhifadhi endelevu wa bonde la Mto Mara upande wa Tanzania, tumekutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wakulima, wachimbaji wadogo wa madini, wavuvi, maafisa mazingira kutoka Serikali za Mitaa (Halmashauri) na viongozi wa dini,” Mratibu wa TNDF, Hadija Malimusi amesema muda mfupi baada ya warsha ya wadau hao mjini Tarime, wiki iliyopita.

Wadau wengine muhimu waliohudhuria warsha hiyo ni viongozi wa Jumuia za Watumiaji Maji katika Bonde la Mto Mara.Akiwasilisha mada katika warsha hiyo, Afisa Mradi wa NELSAP (Nile Equatorial Lakes Subsidiary Action Programme - Mara River Basin Project), Terence Ngoda ametaja uchafuzi wa vyanzo vya maji kuwa ni moja ya matishio ya kimazingira yanayotishia uhai wa bonde hilo.

Aidha, Ngoda amesema kutopatikana kwa takwimu na taarifa za usimamizi wa raslimali za maji katika bonde hilo pia ni moja ya changamoto zinazolikabili.

Ngoda akiwasilisha mada

Ngoda ameongeza kuwa uhifadhi endelevu wa ikolojia ya Serengeti-Masai Mara upo katika hatari kutokana na matishio ya kimazingira yanayoendelea kwenye bonde hilo.

Ametaja changamoto nyingine kuwa ni ukosefu wa maji kwa matumizi ya binadamu katika vijiji na miji midogo iliyopo jirani na Mto Mara.“Tuna tatizo kubwa la ukosefu wa maji katika vijiji vilivyo jirani na bonde na pia tuna tatizo kubwa la uchafuzi wa vyanzo vya maji,” Ngoda amesisitiza.

Tatizo lingine amesema ni ukosefu wa maji kwa shughuli za kiuchumi kama vile kilimo, uvuvi na uzalishaji umeme kwenye maeneo ya bonde hilo ambalo linaripotiwa kusaidia maisha ya watu zaidi ya milioni moja katika nchi za Tanzania na Kenya.Hata hivyo, Ngoda amesema katika kukabiliana na changamoto mbalimbali ndani ya Bonde la Mto Mara, NELSAP ilibuni na kuandaa mradi wa kujenga bwawa katika vijiji vya Borenga (Serengeti) na Mrito (Tarime). Upembuzi yakinifu, usanifu wa mradi, na uandaaji wa makabrasha ya zabuni umekamilika na kukabidhiwa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maji ili mradi huu uweze kuingizwa katika mipango ya Serikali kwa utekelezaji.

Amesema utekelezaji wa mradi huo utakuwa na manufaa mbalimbali kwa wakazi wa Bonde la Mto Mara. Miongoni mwa faida hizo ni kilimo cha umwagiliaji ambapo inakadiriwa hekari 8,340 katika vijiji 13 (10 Serengeti na 3 Butiama) vitaweza kunufaika na kilimo hicho.Bwawa la Borenga/Mrito litatoa huduma ya maji safi na salama kwa vijiji 17 vya wilaya za Butiama, Serengeti na Tarime.

Aidha, uzalishaji wa umeme wa maji 2.8 megawati zitapatikana. Bwawa hilo litasaidia kukabiliana na mafuriko ambayo hugharimu maisha ya watu na mali zao. Mradi huo unatarajiwa kugharimu Dola za Kimarekani zaidi ya milioni 217.“Mpango upo tayari na umekabidhiwa serikalini kwa ajili ya kuutafutia fedha na tuna imani utakuwa suluhisho la matatizo yaliyopo katika Bonde la Mto Mara kwa sasa,” amesema Ngoda ambaye ni mtalaamu wa mazingira aliyebobea kwenye masuala ya maji.

Amesisitiza kuwa shughuli mbadala za kiuchumi zitasaidia kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kuinua hali ya maisha kwa wananchi wanaoishi jirani na bonde hilo.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TNDF, Dkt Donald Kashongi amesema lengo kuu la warsha hiyo ya mashauriano lilikuwa kujadili maendeleo ya usimamizi wa rasilimali za Mto Mara na changamoto zilizopo ili kutafuta njia za kuboresha usimamizi wa rasilimali za maji, upatatikanaji wa taarifa, usawa wa kijinsia na kuweka mikakati zaidi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Dkt Kashongi akiwasilisha mada

“Baadaye kutakuwa na mashauriano ya bonde zima yakihushisa mataifa ya Tanzania na Kenya,” Dkt Kasongi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa NDF amesema.

NDF inaundwa na nchi 10 na makao makuu yake yapo Entebe nchini Uganda.Awali, akizunumza katika warsha hiyo, Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) ya Tarime, John Marwa amewataka wadau wa Bonde la Mto Mara kuendelea kuwa mabalozi wa uhifadhi wa bonde hilo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.

“Maji hayana mbadala, hivyo lazima tutunze vyanzo vya maji,” DAS Marwa amesisitiza.

(Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages