MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Ally Hapi leo ameongoza viongozi mbalimbali wa chama na Serikali, wadau na wananchi kupanda miti zaidi ya 2,000 katika vijjiji vinavyozunguka bwawa la Manchira wilayani Serengeti, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika (kwa sasa Tanzania), yatakayofikia kilele kesho Desemba 9, 2021.
RC Hapi (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Dkt Vicent Mashinji wakipanda miti katika hifadhi ya bwawa la Manchira.
RC Hapi ametumia nafasi hiyo pia kuhimiza wananchi kutunza vyanzo vya maji na kutaka wanaokata miti na kuingiza mifugo katika vyanzo vya bwawa hilo kupewa adhabu kali.
“Miti hii itunzwe kama kielelezo cha maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru. Adhabu ya kuingiza ng’ombe iwe ni kupanda miti 100, kuwepo na mkakati wa kuweka uzio katika bwawa hili na kila kaya ipande angalau miti mitano kwenye chanzo cha maji,” ameagiza.
RC Hapi
Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) limeahidi kuendelea na juhudi za kuhamasisha upandiji miti na uhifadhi mazingira katika eneo kinga na vijiji vinavyozunguka bwawa hilo, ambalo limeigharimu Serikali ya Tanzania mamilioni ya fedha, kwa ajili ya kusambaza huduma ya maji safi kwa wakazi wa mji wa Mugumu na vijiji jirani.
“Sisi kama Bodi ya Maji tutaendelea na shughuli hii ya kupanda miti na kuhifadhi, na tunashukuru wadau wote ambao leo tumeunganisha nguvu kupanda miti katika chanzo hiki cha bwawa la Manchira,” amesema Mhandisi Mwita Mataro ambayo ni Ofisa wa Bodi hiyo katika ofisi ya Musoma.
Mataro akitoa taarifa fupi
Kwa upande wake, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Masana Mwishawa amesema wanavijiji watakaofanya vizuri katika upandaji wa miti eneo la bwawa hilo watapewa zawadi ya kugharimiwa kufanya utalii wa ndani katika hifadhi hiyo.
Mhifadhi Mwishawa akinawa baada ya kupanda mti
RC Hapi pia ametumia fursa hiyo kutangaza shindano la kupanda miti na kuahidi zawadi kwa washindi, lakini akaonya kuwa watakaofanya vibaya wataadhibiwa.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa mkoa ameiagiza Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mugumu (MUGUWASA) kuhakikisha inaunganisha huduma ya maji katika vijiji vyote vinavyozunguka bwawa la Manchira.
“Haina tija kwa watu wa hapa (vijiji jirani na bwawa la Manchira) kukosa maji. Watu walio kwenye chanzo cha maji wawe wanufaika,” RC Hapi amesisitiza.
Baada ya shughuli ya upandaji miti, Mkuu huyo wa mkoa amehutubia mamia ya wakazi wa mji wa Mugumu na vitongojii vyake waliojitokeza katika viwanja vya Right to Play kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru.
(Habari na picha zote: Mara Online News)
No comments:
Post a Comment