NEWS

Friday 3 December 2021

Waziri Jafo afungua Maonesho ya Kilimo Mseto Mara
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muumgano na Mazingira), Selemani Jafo leo Desemba 2, 2021 amefungua Maonesho ya Sita ya Kilimo Mseto yanayofanyika kwa siku tatu mfululizo katika viwanja vya kituo cha ATC kilichopo Bweri, Musoma mkoani Mara.

Maonesho hayo hufanyika kila mwaka yakihusisha wakulima wa mazao tofauti kutoka mikoa mbalimbali nchini, ambapo mwaka huu yameingia katika ngazi ya kimataifa, kutokana na kuhusisha wawakilishi wa Shirika la VI-Agroforestry kutoka nchi za Rwanda, Kenya, Uganda na mwenyeji Tanzania.Lengo la maonesho hayo yenye kaulimbiu inayosema “Kilimo Mseto kwa Uhifadhi wa Mazingira na Kipato”, ni kueneza ujumbe kuhusu mchango wa kilimo mseto katika kuboresha hali ya maisha ya watu na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Katika hotuba yake ya ufunguzi huo, Waziri Jafo amehimiza wananchi wa mkoa wa Mara kuendeleza hali ya utulivu na amani iliyopo, ili mkoa huo uendelee kutumiwa kwa shughuli za kimataifa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi licha ya kupongeza Shirika la Vi-Agroforestry lililoandaa maonesho hayo, ameahidi kuunga mkono jitihada hizo kwa kupanda miti zaidi ya milioni 9, ambapo kila halmashauri itapanda miti milioni 1.5.

Mwenyeji wa maonesho hayo ni Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, kupitia shirika lake la Maendeleo la Inland Development Services (IDS).

VI-Agroforestry ni shirika la kimaendeleo lenye makao makuu nchini Sweden, huku likielekeza nguvu kubwa katika kupambana na umaskini na mabadiliko ya tabianchi.

(Imeandikwa na Mara Online News, Musoma)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages