KATA ya Ifulifu inayoundwa na vijiji vya Kabegi, Kiemba na Nyasaungu katika jimbo la Musoma Vijijini, imepokea kutoka Serikali Kuu shilingi milioni 470, kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa shule ya sekondari yake.
Fedha hizo zimetokana na mkopo uliotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa Serikali ya Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya Kampeni ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19, yenye kaulimbiu inayosema “Pambana na UVIKO-19, Kazi Iendelee”.
Ifulifu ndio kata pekee isiyo na sekondari hadi sasa katika jimbo la Musoma Vijijini, hivyo wanafunzi kutoka kata hiyo wanasoma sekondari za kata jirani za Nyakatende na Mugango.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya Mbunge wa Musoma Vijijini kwa vyombo vya habari juzi, ujenzi wa sekondari ya Ifulifu ulianza 2017 kwa michango ya fedha taslimu na nguvukazi za wanavijiji.
Pia, Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo ameshachangia ujenzi wa sekondari hiyo kwa fedha zake binafsi.
Profesa Sospeter Muhongo
Majengo yaliyokamilishwa kwa nguvu za wanavijiji na Mbunge Muhongo ni vyumba viwili vya madarasa na msingi wa jengo la utawala, lakini pia matofali 1,200 yametengenezwa.
“Wanavijiji na viongozi wa kata ya Ifulifu wanatoa shukrani nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuimbuka kata yao ambayo haina sekondari yake, na ujenzi waliouanza unasuasua kwa ukosefu wa fedha. Fedha zimepatikana - Kazi Iendelee,” imesema taarifa hiyo.
Juzi, Profesa Muhongo alienda kijijini Kabegi kufuatilia ujenzi wa sekondari ya Ifulifu na kujadiliana na viongozi wa kata hiyo kuhusu matumizi bora ya shilingi milioni 470 walizopokea kwa aji ya ujenzi huo.
Profesa Muhongo (mwenye koti katikati) akizungumza na viongozi wa ujenzi wa sekondari ya Ifulifu kijijini Kabegi. |
Pamoja na mambo mengine, mbunge huyo ameelekeza vijiji vya Kabegi na Kiemba vifanye vikao vya wanavijiji kuwaeleza malengo ya fedha hizo na matumizi yake yawekwe wazi kwa wanavijiji.
Pia, amewahimiza wanavijiji kuendelea kuchangia nguvukazi ili miundombinu muhimu ya elimu ipatikane kutokana na fedha hizo, na ujenzi uende kwa kasi kubwa na kwa ubora unaokubalika.
“Ifulifu sekondari ifunguliwe Julai 2022, na wanafunzi wa kidato cha kwanza na kutoka vijiji vya Kabegi na Kiemba waendelee na masomo yao kwenye sekondari yao ya kata,” Professa Muhongo amesisitiza.
(Imeandikwa na Mara Online News)
No comments:
Post a Comment