NEWS

Saturday 22 January 2022

Halmashauri Tarime Vijijini yakabidhi madarasa mapya 122 kwa RC Mara



HALMASHAURI ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) leo Januari 22, 2022 imekabidhi vyumba vipya vya madarasa 122 ya shule za sekondari na shikizi, kwa Mkuu wa Mkoa (RC) Mara, Ally Hapi.

Ujenzi wa madarasa hayo umegharimu shilingi bilioni 2.44 zilizotolewa na Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya kampeni ya maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19.

Makabidhiano ya madarasa hayo yamefanyika sambamba na ukaguzi uliofanywa na RC Hapi katika sekondari za Sirari, Nyamwaga Hill na Ingwe.


RC Hapi (mwenye suti) amekata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa vyumba vinne vya madarasa vilivyojengwa na Jura Tanzania Company Ltd katika sekondari ya Ingwe.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Solomon Shati, kati ya madarasa 122 yaliyojengwa, 116 ni ya shule za sekondari na sita ni ya shule shikizi za msingi.

“Madarasa 116 yamejengwa katika shule za sekondari mbalimbali kwa gharama ya shilingi bilioni 2.32 na madarasa sita ya shule shikizi yamegharimu shilingi milioni 120,” Shati amefafanua.


Vyumba viwili vya madarasa vilivyojengwa na Jura Tanzania Company Ltd katika sekondari ya Sirari

Akizungumza wakati wa mapokezi ya vyumba hivyo, RC Hapi amempongeza Mkurugenzi Shati na wasaidizi wake kwa usimamizi mzuri uliowezesha madarasa hayo kujengwa kwa ubora uliokusudiwa.

“Ninawapongeza kwa kazi nzuri, madarasa ni mazuri, yanapendeza sana. Tumshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha zilizogharimia ujenzi huu na tuendelee kumuunga mkono aendelee kuleta nyingine,” amesema.

Kwa upande mwingine, mkuu huyo wa mkoa amewapongeza wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa kupata madarasa mapya na ya kisasa, huku akitumia nafasi hiyo pia kuwahimiza kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao.



Aidha, RC Hapi amewataka walimu kufundisha kwa bidii na kushirikiana na wazazi kupiga vita utoro wa wanafunzi ili kuondoa alama sifuri katika matokeo ya mitihani ya taifa ya kidato cha nne.

Katika ziara hiyo, ameahidi kutoa misaada ya vifaa vya michezo kwa wanafunzi wa sekondari za Sirari na Ingwe, lakini pia kuchangia saruji mifuko 50 kwa ajili ya ujenzi wa vyoo vya wavulana katika sekondari ya Ingwe.

Mbali na vyumba vya madarasa, mkuu huyo wa mkoa amekagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha afya katika kata ya Bumera na shule mpya ya sekondari ya Nyasaricho.


RC Hapi (wa pili kushoto) akizungumza katika sekondari ya Ingwe ambapo vyumba vinne vya madarasa vimejengwa na Jura Tanzania Company Ltd.

“Ni kazi ya serikali kuleta maendeleo, lakini kubwa zaidi tumshukuru Rais Samia kwa kuleta fedha za miradi hii, tuunge mkono viongozi wa serikali na CCM (chama tawala) ili waongeze ari ya kutafuta hela zaidi za maendeleo,” RC Hapi amesisitiza.

Katika hatua nyingine, RC Hapi amezitaka mamlaka husika kuanza kujenga miundombinu ya barabara, umeme na maji kwenye maeneo ya miradi mipya iliyokamilika na inayoendelea kujengwa wilayani Tarime ili kurahisisha huduma kwa wananchi.

Viongozi waliofuatana na mkuu huyo wa mkoa ni pamoja na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime, Marwa Daudi Ngicho ambaye amempongeza Rais Samia na kuelezea kuridhishwa kwake na kazi nzuri ya ujenzi wa miradi mipya ya maendeleo wilayani.

Mwenyekiti Ngicho (mwenye kofia) akitoa maneno ya pongezi kwa Serikali chini ya Rais Samia kwa kutoa fedha nyingi kugharimia utekelezaji wa miradi ya kisekta wilayani Tarime, lakini pia akimpongeza RC Hapi (mwenye suti) kwa kazi nzuri ya kuhamasisha maendeleo mkoani Mara.

Viongozi wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Simon K. Samwel na Mwenyekiti wa Jumuiya ya CCM ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Wilaya hiyo, Joyce William.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

1 comment:

  1. 1xbet korean casino for bitcoins - Legalbet.co.kr
    1xbet korean casino for bitcoins · 1xbet korean casino for bitcoins 1xbet korea · 1xbet korean casino for bitcoins · 1xbet korean casino for bitcoins · 1xbet korean casino for bitcoins · 1xbet korean

    ReplyDelete

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages