WANANCHI Musoma Vijijini wameombwa kuzipa ushirikiano mamlaka zinazotekeleza miradi ya maendeleo, ikiwemo Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini na Mijini (RUWASA) inayojenga miundombinu ya maji katika vijiji vyao.
Wito huo umetolewa leo na Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo, kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Profesa Muhongo ametaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na ya kutandaza mabomba ya maji kutoka Ziwa Victoria, ukiwemo ule wa Chitare - Makojo.
Kulingana na taarifa hiyo, tenki la maji la ujazo wa lita 75,000 limeshajengwa kijijini Chitare na jingine lenye ujazo wa lita 100,000 limejengwa kijijini Makojo.
“Majaribio yalifanyika na maji yakapatikana. Kwa bahati mbaya transfoma (100 kv) iliungua. TANESCO (Shirika la Taifa la Ugavi wa Umeme Tanzania) wanakaribia kufunga transfoma nyingine hapo,” imeeleza taarifa hiyo.
Pia, mradi wa Suguti - Saragana - Nyambono - Mikuyu umejengewa tenki la ujazo wa lita 200,000 katika kitongoji cha Nyabhelango kijijini Nyambono.
“Transfoma (200 kv) ya kusaidia kusukuma maji kutokea kwenye "booster" iliyojengwa kijijini Chirorwe iliungua. TANESCO wanakaribia kufunga transfoma nyingine,” imeongeza taarifa hiyo.
Kwa upande mwingine, mradi wa Suguti - Bugoji - Kanderema - Kaburabura uliotengewa fedha za mkopo kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa ajili ya mapambano dhidi ya UVIKO-19, umeanza kujengewa tenki la maji la ujazo wa lita 200,000 katika kitongoji cha Nyabhelango kijijini Nyambono.
“Kwa hiyo, kitongoji cha Nyabhelango kitakuwa na matenki mawili ya kusambaza maji katika vijiji vya Suguti, Bugoji, Kanderema na Kaburabura,” imesema taarifa hiyo.
Wakati huo huo, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi zinarekebisha mapungufu yaliyopo kwenye ujenzi wa barabara ya Musoma - Makojo - Busekera kwa kiwango cha lami.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mkandarasi husika ameahidi kuanza kuweka lami kipande cha kilomita tano kabla ya Machi 1, mwaka huu.
(Imeandikwa na Mara Online News)
No comments:
Post a Comment