NEWS

Thursday 27 January 2022

RORYA: Mbunge Chege awapa wakulima tani 10 za mbegu bora za mahindiMBUNGE wa Rorya mkoani Mara, Jafari Chege (wa pili kulia pichani juu), amewapa wakulima msaada wa tani 10 (sawa na kilo 10,000) za mbegu bora za mahindi, zenye thamani ya shilingi milioni 50.

Amekabidhi mbegu hizo leo, kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Chikoka ambaye naye amezikabidhi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, Francis Namaumbo na Afisa Kilimo, Dominick Ndyetabura, kwa ajili ya kuzigawa kwa wakulima husika.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo mjini Utegi, Mbunge Chege amesema ametoa msaada huo kutekeleza ahadi yake ya kuwezesha mapinduzi ya kilimo jimboni Rorya.


Maofisa ugani, watendaji wa kata na vijiji wakifuatilia jambo wakati wa makabidhiano hayo

Mbunge Chege mewataka maofisa ugani na watendaji wa kata na vijiji kusimamia kwa weledi na bila upendeleo ugawaji wa mbegu hizo, ili kufanikisha mashamba darasa yatakayotumika kuhamasisha kilimo cha kisasa na matumizi ya mbegu bora.

Amefafanua kuwa ametoa mbegu hizo kama msaada, lakini kila mkulima atakayepata mgawo atatakiwa kulipia kila kilo moja shilingi 2,500 baada ya mavuno, badala ya bei halisi ya shilingi 6,000.

“Tumeona ni vizuri kugawa mbegu hizi kwa sharti nafuu la kila mkulima kulipia hela kidogo baada ya mavuno, ili mradi huu uendelee kuwezesha wakulima wengine, na itafunguliwa akaunti maalumu ya kuweka fedha hizo,” ameongeza.


Mbunge Chege akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya mbegu hizo. Katikati ni DC Chikoka na kushoto ni DED Namaumbo.

Mkurugenzi Mtendaji, Namaumbo, amemshukuru Mbunge Chege akisema msaada wa mbegu hizo umeanzisha hatua mpya ya kuzalisha chakula cha kujitoseheleza na ziada, lakini pia kupunguza umaskini wilayani Rorya.

Kwa mujibu wa Afisa Kilimo, Ndyetabura, mbegu hizo ni aina ya Faru TZH 538 na TZM 523 zenye uwezo wa kuzalisha mavuno ya magunia zaidi ya 20 kwa kila ekari moja.

Naye Mkuu wa Wilaya, Chikoka amempongeza Mbunge Chege kwa msaada huo na kuahidi kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wa mashamba darasa yatakayoanzishwa kutokana na mbegu hizo.


DC Chikoka akizungumza katika hafla hiyo

“Tutafanya huu mradi uwe wa K tatu, yaani Kuheshimika, Kuaminika na Kukopesheka (KKK). Tutaziambia taasisi za kifedha tutumie mradi huu kukopesheka na tutahakikisha jitihada hizi alizoanzisha Mbunge zinafanikiwa.

“Yeyote atakayechezea huu mradi, huyo atakuwa ameamua kuturudisha nyuma, hivyo tutakula naye sahani moja. Ziara zangu zitaegemea sekta ya kilimo. Watakaofanya vizuri tutawapa zawadi,” Chikoka amesema huku akisisitiza kuwa maofisa ugani wana nafasi kubwa ya kufanikisha mradi huo.

Viongozi wengine walioshiriki hafla ya makabidhiano ya mbegu hizo ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Ores Simba na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Wilaya hiyo, Nagosi Manyonyi.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages