NEWS

Friday 4 February 2022

Kihongosi ahimiza mshikamano UVCCM akikagua miradi Tarime




KATIBU wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Kenani Kihongosi, amewahimiza vijana kudumisha umoja na ushirikiano katika kuhamasisha na kushiriki shughuli za maendeleo ya wananchi.

Kihongosi amesisitiza hayo jana wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na vijana wilayani Tarime, Mara.

Kihongosi (katikati) akivishwa skafu wakati wa mapokezi wilayani Tarime

Akihutubia mkutano wa vijana na wananchi kwa ujumla katika ukumbi wa CMG mjini Tarime, Kihongosi ametumia nafasi hiyo pia kupongeza UVCCM Wilaya ya Tarime chini ya Mwenyekiti wake, Godfrey Francis, kwa mapokezi mazuri na utekelezaji wa miradi ya kuwawezesha kuondokana na utegemezi.

Aidha, Katibu huyo wa UVCCM Taifa ametahadharisha wanachama wa CCM kuepuka rafu za kisiasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa viongozi mbalimbali wa chama hicho tawala.

“Ninawaomba viongozi wa chama, wasijihusishe katika mchakato wa uchaguzi - kwa maana ya kubeba wagombea, chama kitachukuwa hatua kali na tutashughulika kikamilifu na wale wote watakaoenda kinyume na utaratibu wa uchaguzi,” ameonya.



Kwa upande mwingine, Kihongosi amewataka viongozi wa CCM kuhamasisha wananchi kujitokeza kwenye sensa ya watu na makazi baadaye mwaka huu, ili kuwezesha serikali kujipanga kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.

Naye Mwenyekiti wa UVCCM Tarime, Godfrey amemshukuru Kihongosi kwa ziara hiyo akisema imeongeza chachu kwa vijana kuondokana na utegemezi kwa maslahi mapana ya Taifa.


Godfrey akizungumza mkutanoni

“Nakushukuru ndugu Katibu wa UVCCM Taifa kwa kutembelea miradi iliyoanzishwa na Umoja wa Vijana wa CCM Tarime na tunakuahidi ushirikishaji zaidi kwa vijana ili waweze kunufaika na fursa zipatikanazo ndani ya wilaya ya Tarime,” Godfrey amesema.

Pia, Kihongosi ametembelea na kuzindua mashina ya CCM katika matawi ya sabasaba na Mwangaza, miradi ya ufugaji samaki na nyuki inayoendeshwa na UVCCM Kiterere - Bumera, lakini pia maendeleo ya ujenzi wa kituo cha afya kata ya Bumera na shamba linaloandaliwa na umoja huo katani hapo.


Katika ziara, Kihongosi amefuatana na wajumbe wa Baraza Kuu Taifa, Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na UVCCM Taifa.

Viongozi wengine ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime, Marwa Daudi Ngicho, Mbunge wa Tarime Mjini, Michael Kembakina Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime mji, Daniel Komote, miongoni mwa wengine.

(Habari na picha zote: Geofrey John)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages