NEWS

Monday 14 February 2022

Maji Safi Group wazindua klabu za hedhi salama kwa wanafunzi, wagawa vifaa vya kujisitiri shuleni


SHIRIKA la Maji Safi Group limezindua klabu za hedhi salama kwa wanafunzi wa shule za sekondari wilayani Butiama, Mara na kugawa vifaa vya kujifunzia na kujisitiri wakati wa hedhi.

Uzinduzi huo umefanyika Ijumaa iliyopita katika shule za sekondari Kukirango, Kyanyari na Kiabakari, lengo likiwa kuvunja ukimya kwa watoto wa kike na kutokomeza utoro shuleni.


Viongozi wa Maji Safi Group, walimu na wanafunzi wakati wa uzinduzi wa klabu za hedhi salama na ugawaji taulo za kike katika Shule ya Sekondari Kiabakari

Mkurugenzi wa Operesheni wa shirika hilo, Rachel Stephen amegawa taulo za kike na vifaa vya kujifunza namna ya kujisitiri wakati wa hedhi kwa wanachama wa klabu hizo.

“Leo tumezindua kilabu tatu kati ya sita, jana tulizindua nyingine tatu na kugawa vifaa vya kujifunzia suala la hedhi salama, kila klabu ina wanachama 60 wakiwemo wavulana 20. Kaulimbiu yetu ni “Hedhi yangu fahari yangu, vunja ukimya,” Rachel amesema.


Rachel Stephen

Mbali na kugawa vifaa mbalimbali kama soksi kwa wavulana, taulo za kike na nguo za ndani kwa wasichana hao, shirika la Maji Safi Group pia limetoa vitendea kazi kama kalamu na madaftari, huku likihimiza wanafunzi hao kuhudhuria vipindi vyote vya masomo darasani.

Meneja Programme wa Maji Safi Group, Rebecca Oyugi amesema kilabu hizo zitawezesha wanafunzi hao kupata elimu ya balehe na hedhi salama, kupunguza utoro unaotokana na hedhi, hivyo kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa kike.“Klabu hizi zitawajengea wanafunzi wa kike na kiume uwezo wa kujitambua, kujilinda dhidi ya ndoa za utotoni, ukatili wa kijinsia, kuondoa unyanyapaa unaotokana na hedhi, kujua mabadiliko ya mwili na hedhi,” Oyugi ameongeza.

Amesema lengo kuu ni kutengeneza mabalozi wa elimu ya hedhi watakaokuwa wawezeshaji kwa wanafunzi wengine na wasimamizi wa usafi wa mazingira shuleni, kuwezesha wanafunzi kuvunja ukimya na kuelimisha athari za mila potofu kuhusu hedhi katika jamii.

Naye Mkuu Msaidizi wa Shule ya Sekondari Kukirango, Mwalimu Annamaria Samson amelipongeza shirika la Maji Safi Group akisema mafunzo hayo yamehamasisha shule yao kuanzisha utaratibu wa kununua taulo za kike kwa ajili ya kugawia wanafunzi wanaoingia hedhi wakiwa shuleni.


“Kwa kweli mafunzo yao yametusaidia, tuliporudi tulitoa semina kwa walimu wote, Mkuu wa Shule akatuelewa, sasa hivi hutoa shilingi 23,000 za kununua boksi la taulo za kike, kopo la panado na dawa za mchafuko wa tumbo kwa watoto wa kike wanapoingia hedhi hapa shuleni na tayari tumewatengea chumba maalumu,” Mwalimu Annamaria amesema.

Hata hivyo, mwalimu huyo ametumia nafasi hiyo pia kuiomba serikali kuwajengea wanafunzi wa kike vyoo maalumu kwa ajili ya huduma za kujisitiri wanapokuwa kwenye hedhi.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages