NEWS

Saturday 19 February 2022

Wanavyuo 120 kutoka Mwanza wafanya utalii wa ndani Serengeti



WANAVYUO 120 (wanafunzi 107 na walimu 13) kutoka mkoani Mwanza, wamefungua ukurasa mpya kwa kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, kujionea vivutio vinavyoipamba hifadhi hiyo.

Wakitokea chuo cha udaktari na ufamasia cha City College, Chuo cha Kilimo Ukirigulu na Chuo cha Mipango, wanavyuo hao wamepokewa leo Februari 19, 2022 katika lango la Ndabaka na Afisa Mhifadhi Mkuu, Augustino Masesa.

Mmoja wa viongozi wa msafara huo, Sebastian Mohamed amesema wameamua kutembelea Hifadhi ya Serengeti baada ya kuhamasishwa katika kongamano la wanavyuo vikuu na vya kati lililoandaliwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na kufanyika jijini Mwanza mwezi uliopita, ambapo mgeni rasmi alikuwa Kamishna Mwandamizi wa Uhifadhi Kanda ya Magharibi, Martin Loibooki.


Makundi ya wanyamapori ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti

“Tumeona sisi kama Watanzania, lakini pia kama vijana tuje kutembelea vivutio vyetu vya utalii ambavyo Mwenyezi Mungu ametujaalia, ili tuweze kujifunza mambo mengi kuhusu wanyamapori na mazingira hai badala ya kusimuliwa.

“Mimi nimefika leo kwa mara ya kwanza baada ya kupata hamasa kwenye kongamano la kuhamasisha utalii wa ndani kupitia wanavyuo lililofanyika jijini Mwanza,” amesema Mohamed na kuendelea:

“Serengeti ni mbuga kubwa, ninapenda kutoa wito kwa wanavyuo wengine, Watanzania wote kutoka mikoa jirani, Kanda ya Ziwa na Tanzania kwa ujumla, waje kujionea mema tuliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu katika hifadhi hii ya Serengeti, gharama ni nafuu sana kwa mtalii wa ndani.”

Kwa upande wake, Mhifadhi Masesa amewashukuru na kuwapongeza wanavyuo hao kwa kuhamasika kutembelea hifadhi hiyo na kuwatakia utalii wa ndani wenye fanaka hifadhini.


Mhifadhi Masesa (wa tatu kushoto) katika picha ya pamoja na baadhi ya wanavyuo hao

Mhifadhi huyo amesema matumaini yake ni kwamba baada ya ziara hiyo, wanavyuo hao watakuwa mabalozi wa kutangaza utalii wa ndani katika vyuo vyao na maeneo watakayofanya kazi baada ya kuhitimu masomo yao.

Ametumia nafasi hiyo pia kuwakaribisha wanavyuo na Watanzania wengine kuitembelea hifadhi hiyo, akisema Hifadhi ya Serengeti ni kivutio cha kipekee na imetunukiwa tuzo ya hifadhi bora Afrika kwa miaka mitatu mfululizo (2019, 2020 na 2021).

“Ni fursa kubwa kwa Mtanzania kuitembelea Hifadhi ya Serengeti kama mtalii wa ndani. Tunaendelea kuhamasisha utalii wa ndani kupitia makongamano na semina kwenye mashirika na taasisi mbalimbali zikiwemo shule,” Mhifadhi Masesa amesema.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages