NEWS

Friday 11 February 2022

DC Serengeti afungua mafunzo ya kukabili migogoro ya binadamu-wanyamapori

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti (DC) Dkt Vincent Mashinji leo Februari 11,2022 amefungua mafunzo yenye lengo la kukabiliana na migogoro ya binadamu na wanyamapori katika wilaya hiyo ambayo sehemu yake kubwa inapakana na ikolojia ya Serengeti.

Mafunzo hayo ya siku tano yameandaliwa na Shirika la kimataifa la Uhifadhi la Frankfurt Zoological Society (FZS) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania(TAWIRI) na kuhudhuriwa pia na wadau muhimu wa uhifadhi katika wilaya hiyo.

Dkt Mashinji ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuacha tabia ya kugeuza maeneo yaliyohifadhiwa kuwa malisho ya mifugo huku akisisitiza kuwa ikolojia ya Serengeti lazima ihifadhiwe na kulindwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

“Tusipeleke mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa. Kuna migogoro mingine tunaitengeneza sisi”, alionya Mkuu huyo wa wilaya.

Amesema kuwa uhifadhi na ulinzi
wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni kipaumbele cha Serikali ya Tanzania.

“Hatutakubali Serengeti ipotee, uhifadhi na ulinzi wa Serengeti ni kipaumbele cha kwanza”, amesisitiza Dkt Mashinji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayub Mwita Makuruma amepongeza shirika la FZS kwa kuandaa mafunzo hayo ya nadharia na vitendo(pracitical) na kuomba mpango huo uwe endelevu.
“Sisi hifadhi tunaipenda sana na ninaomba huu mpango wa kutoa mafunzo ya kuzuia migogoro ya wanyamapori na binadamu uwe endelevu “, amesema Makuruma.

Mbali na mafunzo hayo shirika la FZS lenye makao makuu yake nchini Ujerumani limetoa msaada wa vifaa mbalimbali vikiwemo vile vitakavyo wezesha wanufaika wa mafunzo hayo kufukuza Wanyama waharibifu hususani tembo ambao wamekuwa wakila mazao.

Baadhi ya vifaa hivyo ni simu maalumu ambazo zitaweza kusaidia kufuatilia wanyamapori waharibufu na kutoa taarifa kwa ajili ya kuzuia madhara yanayosababishwa na migogoro hiyo, kompyuta mpakato, tochi , darubini na vuvuzela.

Awali Meneja Mradi wa FZS, Masegeri Rurai amesema mafunzo hayo yamelenga vijiji saba ambavyo vinaunda Jumuiya ya Wanyamapori(WMA) ya Ikona na vijiji vingine vinne ambavyo viko nje ya WMA hiyo.
“Lengo hasa ni kuwa na mbinu sahihi na rafiki ili kupunguza na kuzuia madhara ya wanyamapori waharibifu “,amesema Masegeri.

Masegeri amesisitiza pia umuhimu wa kutumia mbinu za kiasili katika kukabiliana na changamoto hiyo ambayo pia inaripotiwa kuongezeka baada ya idadi ya wanyamapori kuongezaka kutokana na juhudi za uhifadhi zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalibali katika ikolojia ya Serengeti.

Alitaja vijiji ambavyo vitanufaika na mafunzo hayo kuwa ni Robanda, Park Nyigoti, Nyanungu, Makundusi, Natta-mbiso ambavyo viko kwenye eneo la Ikona WMA.

Vijiji vingine vinne ambavyo vipo nje ya WMA ni Motukeri, Singisi, Iharara na Nyiberekera.

Kwa upande wake Dr Janemary Antalwila ambaye ni mkuu wa kitengo cha habari na elimu kutoka TAWIRI amesema mbinu zitakazotolewa kwa washiriki wa mafunzo hayo zitasaidia kupunguza migongano kati ya binadamu na wanyamapori katika vijiji hivyo.
“ Lengo ni kuonesha kuwa binadamu na wanyamapori wanaweza kuishi pamoja na tuna imani mbinu tunazotoa zitasadia kupunguza changamoto iliyopo”, alisema Dr Janemary.

Takwimu zinaonesha Serengeti inaongoza kwa kuwa na matukio mengi ya migogoro kati ya binadamu na wanyamapori nchini, kwa mujibu wa Dr Janemary.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages