MWENYEKITI wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kutakuwepo umakini mkubwa katika kufuatilia mwenendo wa wanachama kuelekea uchaguzi wa viongozi wa chama hicho na jumuiya zake.
“Hapa Mara tumeona pilika pilika hizo, lakini jicho la Chama litakuwa wazi kuangalia yanayojitokeza,” Rais Samia amesema katika sehemu ya hotuba yake leo Februari 5, 2022 kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 45 ya kuzaliwa kwa CCM, yanayofanyika kitaifa Musoma mkoani Mara.
Kiongozi huyo wa nchi amesema kila mwanachama ana haki ya kugombea, lakini uongozi ndani ya chama hicho haitakiwi utumike kama mwanya wa kujipatia maslahi binafsi.
Ametaka uchaguzi huo wenye kaulimbiu inayosema “CCM Imara, Shiriki Uchaguzi kwa Uadilifu”, ufanyike kwa viwango vilivyotamalaki haki na uadilifu.
Vijana wa Halaiki wakipamba maadhimisho hayo kwa nyimbo za kizalendo
Rais Samia ametumia nafasi hiyo pia kuipongeza Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM - chini ya Katibu Mkuu, Daniel Chongolo, kwa kazi nzuri ya kufuatilia utekelezaji wa ilani ya chama hicho ya mwaka 2020 - 2025.
Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa amesema serikali itaendelea kutekeleza ilani hiyo kwa bidii, maarifa, nguvu na uaminifu wote, ili kuwaletea wananchi maendeleo endelevu ya kisekta na kuinua ustawi wa maisha yao.
Amewataka Watanzania kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini, huku wakifanya kazi kwa bidii kupiga vita maadui umaskini, maradhi na ujinga.
Kwa upande mwingine, Rais Samia amehimiza Watanzania kushiriki katika sensa ya watu na makazi itakayofanyika baadaye mwaka huu.
(Imeandikwa na Mara Online News)
No comments:
Post a Comment