MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeendesha semina kwa wafanyabiashara wilayani Tarime, Mara ambapo imesisitiza umuhimu wa kulipa kodi kwa wakati na matumizi ya Mashine Maalum za Kielekroniki (EFDs) kuepuka usumbufu.
Akizungumza katika semina hiyo mjini Tarime leo Februari 9, 2022, Afisa Elimu na Huduma kwa Mlipakodi kutoka TRA Makao Makuu, Tshaka Shariff pia amekemea vitendo vya magendo, kwani vinaikosesha serikali mapato.
Hata hivyo, wafanyabiashara hao wameshauri serikali kujenga viwanda, kikiwemo cha sukari wilayani Tarime kama suluhisho thabiti la tatizo la magendo mpakani na nchi ya Kenya.
Kuhusu mashine za EFD, wameshauri TRA kuanzisha kitengo cha kuzifanyia marekebisho kwenye ofisi zao za wilayani, ili kuwaondolea usumbufu wa kuzipeleka kurekebishwa katika mikoa ya mbali.
Aidha, wafanyabiashara hao wameomba Mamlaka hiyo kutoa huduma kwa wakati na kulegeza masharti ili kuwezesha wengi kulipa kodi.
“Tunaomba mpunguze masharti watu walipe kodi,” amesema Boniface Nyablangeti.
Katika semina hiyo, Shariff amefuatana na Afisa Mwandamizi wa Kodi kutoka Makao Makuu, Julieth Kidemi na Sigsimund Kafumu kutoka Musoma, miongoni mwa maofisa wengine wa TRA.
(Habari na picha zote: Mara Online News)
No comments:
Post a Comment