NEWS

Thursday 10 February 2022

Wadau wajadili maendeleo Tarime, DC akemea ubaguzi wanafunzi shuleni
WADAU mbalimbali wamekutana katika Kikao cha Ushauri cha Wilaya (DCC) ya Tarime kujadili maendeleo ya kisekta ya wilaya hiyo.

Kikao hicho kimefanyika ukumbi wa TTC mjini Tarime leo Februari 10, 2022, kikiongozwa na Mkuu wa Wilaya (DC), Kanali Michael Mntenjele (mwenye shati nyeupe pichani juu).

DC Mntenjele ametumia nafasi hiyo kupiga marufuku kasumba iliyojengeka katika baadhi ya shule za msingi na sekondari - ya kuwachangisha fedha wazazi wa wanafunzi wanaotoka nje ya kijiji, au kata husika, akisema huo ni ubaguzi usiokubalika nchini.

“Huo ubaguzi mnautoa wapi? Shule ikishakuwa ya serikali ni ya umma, mtoto yeyote kutoka Tanzania atasoma kwa utaratibu ule ule wa wenyeji.

“Kama ni mchango wa chakula wazazi wenyewe wachangishane na kusimamia wenyewe - siyo shule, na hakuna kubaguana kwamba shule hii ni yetu - wanaotoka nje ya kijiji wachangie. Huo ubaguzi hauko Tanzania,” DC Mntenjele amesisitiza.

Amesema kitendo cha kumpa mazazi masharti ya kuchanga fedha kwa kigenzo kwamba mtoto wake anatoka nje ya eneo ilipo shule, ni adhabu ya uonevu - inayolenga kumnyima mtoto haki ya kupata elimu.

Wajumbe kikaoni

Kwa upande mwingine, kiongozi huyo ameitaka Halmashauri ya Mji wa Tarime kutenga eneo maalumu nje ya mji, kwa ajili ya maegesho ya malori makubwa, ili kuepusha msongamano na uharibifu wa barabara katikati ya mji.

Mkuu huyo wa wilaya ametumia nafasi hiyo pia kuwataka wananchi kutowalinda wahalifu katika maeneo yao, badala yake wawafichue ili vyombo vya ulinzi na usalama viwachukulie hatua za kisheria.

Katika hatua nyingine, DC Mntejele amewakumbusha viongozi wa kisiasa, wakiwemo wabunge na madiwani kuisaidia serikali kuhamasisha wananchi wajitokeze kutoa taarifa sahihi wakati wa utekelezaji wa mpango wa anuani za makazi - kama ilivyosisitizwa na Rais Samia Suluhu Hassan, hivi karibuni.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime, Marwa Daudi Ngicho amewapongeza viongozi wa halmashauri za Mji na Wilaya ya Tarime, kwa kusimamia na kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa ya shule za sekondari na shikizi kwa ufanisi.

Ngicho akizungumza kikaoni

Katika DCC hiyo, halmashauri za Mji na Wilaya ya Tarime, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Wilaya ya Tarime, zimewasilisha taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mwaka 2021/2022 na makisio ya mapato na matumizi kwa 2022/2023.

Kikao hicho kimehudhuriwa na viongozi wa serikali, madhehebu ya dini na taasisi mbalimbali, wakiwemo Katibu Tawala wa Wilaya, John Marwa, Wenyeviti wa Halmashauri, Daniel Komote (Tarime Mji) na Simon K Samwel (Tarime Vijijini).

Wengine ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Gimbana Ntavyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), Solomon Shati na Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Viwanda na Kilimo (TCCIA) Tarime, Chacha Kisengewa.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages