NEWS

Saturday, 19 March 2022

Kamati ya Waziri Jafo yasema maji ya mto Mara ni salama



KAMATI ya Kitaifa ya Watu 11 iliyoundwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu ya Rais (Muungano na Mazingira), Seleman Jafo (pichani juu katikati) kuchunguza chanzo cha uchafuzi wa mto Mara, imesema maji ya mto huo ni salama na hayawezi kuathiri afya za binadamu.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Profesa Samwel Manyele (pichani juu kulia) ameyasema hayo katika taarifa ya matokeo ya uchunguzi, wakati akiiwasilisha kwa Waziri Jafo katika kikao kilichohudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi (pichani juu kushoto) mjini Musoma, leo Machi 19, 2022.

Hata hivyo, Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na mamlaka za maji mkoani Mara zimetakiwa kuweka mkakati wa kutibu maji ya mto huo kabla ya kunywa, kama ilivyopendekezwa na kamati hiyo.

Profesa Manyele amesema katika taarifa hiyo kwamba uchunguzi walioufanya umebaini chanzo cha uchafuzi ulioripotiwa kutokea katika mto huo ni nguvu za asili, kinyesi cha mifugo na uozo wa mimea.

Ameongeza kuwa wamebaini katika eneo oevu la mto Mara lenye ukubwa wa kilomita za mraba 423 kumekuwa na shughuli za kilimo na ufugaji.

“Katika eneo hili kulikuwa na ng’ombe zaidi ya laki tatu waliokaa hapo kwa zaidi ya miezi minane na hadi wakati uchunguzi unafanyika bado kuna ng’ombe kiasi pamoja na ushahidi kuwa wakati wa kiangazi watu huwa wanaishi katika eneo hilo,” amesema.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wakati wa kiangazi wafugaji katika mikoa ya Kanda ya Ziwa huweka ng’ombe wao kwenye eneo hilo oevu kwa ajili ya malisho na maji, limesababisha uwepo wa mlundikano wa kinyesi, mkojo na maozea ya uoto wa asili wa mto huo.

Profesa Manyele amesema uchunguzi wao umehusisha pia mahojiano na wananchi, wakiwemo wakulima, wafugaji, wavuvi, wachimba madini, wananchi wanaoishi kando kando ya mto Mara na wataalamu mbalimbali.

Taarifa ya uchunguzi wa kitaalamu imebaini pia uwepo wa mafuta yaliyotokana na uozo wa mimea (decomposition) katika eneo oevu la mto Mara, hali iliyochangia uchafuzi wa mto huo.

Lakini mafuta hayo, kwa mujibu wa taarifa hiyo, hayatokani na miamba ya aridhini.

Aidha, imefafanua kuwa kinyesi cha ng’ombe kilitifuliwa na mvua kubwa iliyonyesha hivi karibuni na kutiririkia mto Mara. Hivyo kuoza kwa mimea na kinyesi cha ng’ombe vilisababisha rangi ya maji kubadilika kuwa nyeusi na kusababisha harufu mbaya.

Imeongeza kuwa samaki walikufa katika mto huo baada ya kukosa hewa ya oksijeni kutokana na mafuta yaliyotokana na kuoza kwa mimea na maji kubadilika rangi, hivyo kushindwa kupokea mwanga wa jua.

Kuhusu usalama wa maji amesema hapakuwa na sumu na kwamba kemikali zote ndani ya maji zipo kwenye kiwango kinachotakiwa, hivyo wananchi wanaruhusiwa kutumia maji isipokuwa kwa ajili ya kunywa lazima yatibiwe.

Pia, ni rukusa kwa watu kutumia samaki wa mto Mara, kwani uchunguzi wa kimaabara umebaini hakuna sumu katika mto huo.

Uchunguzi huo ulilenga kubaini chanzo cha uchafuzi wa mto Mara baadhi ya maeneo, yakiwemo ya kijiji cha Marasibora wilayani Rorya na Wegero wilayani Butiama.

Kamati ya uchunguzi huo iliongozwa na Profesa Manyele kutoka Idara ya Uhandisi wa Kemikali na Madini Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Katibu wa Kamati hiyo, Dkt Samuel Gwamaka ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Wajumbe wa kamati hiyo ni Dkt Kessy Kilulya, Mkuu wa Idara ya Kemia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt Kessy Kilulya, Dkt. Charles Kasanzu kutoka Idara ya Jiolojia UDSM, Mkurugenzi wa Udhibiti na Usimamizi wa Kemikali Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Daniel Ndio na Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB), Mhandisi Renatus Shinhu.

Wengine ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Samaki (TAFIRI) Mwanza, Baraka Sekadende, Dkt Neduvoto Mollel kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Usimamizi wa Viuatilifu (TPHPA), Afisa kutoka Ofisi ya Rais Ikulu, Yusuf Kuwaya kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Faraja Ngelageza ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi Bioanuai kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages